Serikali ya Saudi Arabia imepiga marufuku uchukuaji wa picha za Selfie au video katika maeneo ya msikiti mtakatifu wa Makkah pamoja na Msikiti wa Mtumeﷺ masjid Nabaw
ulioko mji wa Madina.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa marufuku hiyo imeanza kufanya kazi tangu Novemba 12 mwaka huu.
Taarifa hiyo ilitolewa na wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia kupitia barua ya kidiplomasia iliyopelekwa kwa mabalozi wa nchi kadhaa wenye wawakilishi nchini Saudi
Arabia.
Mamlaka ya Saudi Arabia ilisema zuio hilo ni katika kulinda na kuhifadhi maeneo matakatifu kwa kuzuia mvutano kwa waumini na kuhakikisha utulivu wakati wa ufanyaji ibada katika maeneo hayo matakatifu.
Taarifa hiyo inasema yeyote atakayekiuka marufu hiyo, walinzi wa usalama wameagizwa kuchua picha au kamera kama itaonekana inafaa kufanya hivyo.
Pia taarifa hiyo imesisitiza kusambazwa kwa kila taasisi zinazopeleka Mahujaji katika ibada ya Hija na Umra katika nchi mbalimbali.
Zuio hilo limepokewa kwa hisia tofauti na watu wa makundi kadhaa. Wapo wanaoona zuio hilo ni sahihi na wengine wanaona sio sahihi.
Wengine wameomba mamlaka ya Saudia kupanga maeneo maalumu ya kupiga picha na wasiweke zuio la moja kwa moja kwani wengi wamekuwa wakifanya hivyo kama sehemu ya kumbukumbu katika maisha yao.
Baadhi wanaamini kuwa tabia hiyo inaweza kuwa kizuizi cha kufikia unyenyekevu na utulivu wakati wa kufanya matendo ya ibada, hasa wakati wa ibada ya hija na Umra.
Nini maoni yako kuhusu zuio hilo. Je ni sawa au si sawa.
SELFIE YAWAKERA BAADHI YA WASOMI KATIKA IBADA YA HIJJA