Sunday, 26 February 2017

MUDIR SHAMSUL MAARIFA AKABIDHIWA SHALI YA ZAMA NA SHARIF MIHDHWARI KHITAMY

MUDIR wa Mahdi (Chuo) Shamsul Maarifa ya Tanga Sheikh Samir Sadiq jana alituzwa na kutunikiwa Shali na Sharif Mihdhwar Abdulrahman Khitamy wa Kenya.

Tukio hilo la aina yake lilifanyika katika shughuli ya hauli ya Sheikh Muhammad Bakar aliyekuwa Mudir wa Mahdi(chuo kikuu) Shamsul Maarif aliyefariki dunia usiku wa Jumatatu ya tarehe 7 mwezi wa Machi mwaka 2016 jijini Dar es Salaam.
Shali (kilemba/kashda) ni kitambaa kizito cha Sufu cha kuweka mabegani na mara nyingi huvaliwa na wanazuoni wa kiislamu. 
Aidha shali za namna hiyo hurithishwa kutoka kwa wanazuoni wema kutoka kwa mmoja baada ya mwingine.
Kutuzwa na kupewa Shali hiyo kwa Sheikh Samir ni dalili na alama ya kukubalika kwake kwa Elimu na uadilifu. 
Hata hivyo Sharif Mihdhwari hakutaka kutaja nasabu ya Shali hiyo bali alieleza kwamba ni moja ya mabaki ya watu (wanazuoni) wa zamani sana na ndani ya shali hiyo kuna utulivu.
Sharif Khitamy kushoto na Sheikh Muhammad Bakar kulia. Kwa nyuma Shari Mihdhwari
Tukio kama hilo liliwahi kufanyika mwaka 2004 chuoni hapo wakati Baba yake Sharif Mihdhwari, Sharif Abdulrahman Khitamy alipomvesha Sheikh Muhammad Bakar Shali, wakati wa ufunguzi wa Msikiti Bajabir uliopo chuoni hapo.

Baada ya miaka 12 watoto wa wanazuoni wamekuja kufuata nyayo za wazazi wao. Sharif Mihdhwari ni mtoto wa damu wa Sharif Abdulrahman Khitamy na Sheikh Samir ni Mtoto wa kielimu wa Sheikh Muhammad Bakar.
Hauli hiyo iliyoanza Alasiri mpaka Magharibi ilihudhuriwa na Masheikh wengi wa kutoka sehemu mbalimbali akiwemo Naibu Kadhi wa Comoro (Mjukuu wa alhadad), mtoto wa Sheikh Muhammad Albeidh Sharif Jaafar, Sheikh Kiungiza na wengine wengi.