Monday, 9 January 2017

AUSTRIA KUPIGA MARUFUKU UVAAJI WA HIJABU

Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria ambaye anashughulikia masuala ya namna wahajiri wa kigeni, Sebastian Kurs ametoa wito kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na walimu wa shule marufuku ya uvaaji wa Hijabu katika maeneo ya umma.
Sebastian Kurs anayetoka chama cha Christian Conservative People's Party (OVP) anashirikiana na waziri mwenzake Mwislamu, Muna Duzdar, ambaye ni Waziri wa Huduma za Umma na Mfumo wa Dijitali kutengeneza sheria ya upigaji marufuku uvaaji wa Hijabu.

Wafanyakazi wote wa umma Austira, wakiwemo walimu, watapigwa marufuku kuvaa Hijabu wakiwa kazini.

Sheria ya kupiga marufuku vazi la Hijabu inatayarishwa na Sebastian Kurs, Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria ambaye pia anashughulikia masuala ya namna wahajiri wa kigeni wanavyopaswa kufuata ustamaduni wa nchi hiyo.

Duzdar amedai kuwa sheria hiyo inalenga kuibua mazungumzo na maelewano baina ya wafuasi wa dini zote.

Waislamu wa nchi Austria wamelalamikia vikali mpango wa kuwapiga marufuku kuvaa vazi la staha la Hijabu katika maeneo ya kazi za umma.

Waislamu wa Austria wamemtaka Sebastian Kurz, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kufanya mazungumzo nao, kuhusiana na marufuku hiyo katika maeneo ya umma.

Omral Rawi, mkuu wa jopo kuu taasisi ya Waislamu wa Austria amesema, serikali na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, bila ya shaka wanahitajia uungaji mkono wa Waislamu.

Naye mshauri wa serikali ya Austria na baadhi ya weledi wa mambo wamependekeza kuwa, kuna wajibu wa kujadiliwa kwa kina marufuku hiyo ya Hijabu kabla ya kuingizwa katika sheria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria alitangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo ina nia ya kuwapiga marufuku Waislamu kuvaa vazi la staha la Hijabu katika maeneo ya umma wakiwemo walimu mashuleni.

Hivi sasa chama cha kihafidhina cha Austria kinaandaa muswada wa kuifanya marufuku hiyo kuwa sheria. Iwapo muswada huo utapitishwa na bunge la nchi hiyo, Waislamu watazidi kunyanyaswa katika nchi hiyo ya Ulaya.

Austria inajiunga na Ufaransa ambayo imepiga marufuku vazi la staha la Hijabu huku kukiwa na chuki dhidi ya Waislamu hasa wanawake wanaovaa Hijabu katika nchi mbali mbali za Ulaya na Amerika ya Kaskazini.