Monday, 12 December 2016

WAZIRI MWIGULU NCHEMBA: 'ALIYESHIKA DINI YAKE SI MDINI NI MCHA MUNGU, ANAYEFANYA KOSA AHUKUHUMIWE KWA KOSA LAKE NA SIO DINI YAKE'

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba amesema yeyote anayefanya kosa ahukumiwe aliyetenda bila ya kuihusisha dini yake.
Aidha aliongeza kusema kuwa watu watofautishe kati ya mcha mungu na mdini.

Waziri Nchemba aliyasema hayo leo katika sherehe za Baraza la Maulid lililofanyika kitaifa Shelui, Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.  

Sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad kitaifa huadhimishwa kila mwaka ifikapo mfungo sita (Rabiul awwal) mwezi 12 na Kauli mbiu ya Maulid ya mwaka huu ni "Muislamu jitambue badilika amani na usalama ndiyo maisha yetu”.

"Tutofautishe udini na kumcha mungu. Mtu anaposhika sana dini yake si mdini ila ni mcha mungu", alisema waziri Nchemba na kuendelea, "Mdini ni mtu anayebeza dini nyingine, anayebagua watu kwa misingi ya dini, anayependelea watu ama kudharau watu kwa misingi ya dini."

Aliongeza kusema, "Kumekuwepo na tatizo mtu akionekana ameshika sana dini yake, anaswali sana ama anashinda msikitini anahusishwa na siasa kali, anahusishwa na udini. Na wengine ndio wanaopakaziwa kwamba huyo lazima atakuwa gaidi tu, aishi msikitini?

Aliendelea kufafanua kwamba, "kumcha mungu kwa kadri ya kitabu chako kinavyoeleza si udini, ni Ucha Mungu."

Jambo la pili alilolizungumza ni kwamba makosa yote katika nchi yatafanywa na watu aidha wenye dini au wasio na dini hivyo akasema ahukumumiwe mtu kwa kosa lake na si dini yake.

"kosa lolote litakalofanywa na mtu yeyote, liwe kosa la yule mtu, si kosa la dini yake. Kama ambavyo mtu mwenye kabila moja akifanya kosa haliwi kosa la kabila, linakuwa kosa la yule aliyefanya kosa hilo", alisema Waziri Nchemba.

Aliongeza kusema ikiwa mkristo au mwenye jina la kiislamu amefanya kosa zisihukumiwe dini zao kwani jamii ikitambua hivyo itasaidia nchi kuwa yenye dini mbalimbali zenye uhuru wa kuabudu na kuishi kwa kuelewana.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo za Baraza la Maulid alikuwa ni Waziri mkuu Kassim Majaliwa. 

Wengine waliohudhuria ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano Mheshimiwa January Makamba, Naibu Waziri ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jaffo, Mbunge Lazaro Nyalandu, Mkuu wa Mkoa Singida Rehema Nchimbi na wengine wengi wakiwemo Masheikh na viongozi wa kitaifa.