Hospitali ya kwanza yenye kufuata taratibu, Sharia na adabu za kiisalmu inatarajiwa kuanza huduma zake mwaka 2020 huko Penang, kaskazini magharibi mwa pwani ya Malaysia.
Hospitali hiyo itakayojengwa mji wa Bayan Baru itagharimu pesa za Malaysia RM280 milioni sawa na shilingi Bilioni 137.2 za kitanzania.
Hospitali hiyo itakayofahamika kama The Penang Islamic Hospital (HIPP) inajengwa kwa ushirikiano wa Penang Islamic Foundation (YIPP) na the Penang Islamic Religious Council.
Mwenyekiti wa YIPP daktari Mansour Othman alisema licha ya hospitali hiyo kufuata taratibu za kiislamu lakini itatoa huduma kwa wananchi wote bila ya kujali dini zao.
Alisema kuanzishwa kwa Hospitali hiyo kutachangia ukuaji wa uchumi kwa kutoa ajira mbalimbali kwa watu zaidi ya 1,000.
Aidha waziri kiongozi Daktari Mohd Rashid Hasnon alipongeza kuanzishwa kwa Hospitali hiyo kwa kusema itasaidia sana wananchi na kuwa kitovu cha matibabu kwa nchi za Indonesia na Malaysia na Thailand.
Aliongeza kuwa Hospitali hiyo itapunguza malalamiko ya waislamu kwa kuwa itakuwa inaendeshwa kwa taratibu za kiislamu.
Jengo hilo linatarajiwa kuwa na ghorofa 14 na vitanda zaidi ya 200, litakuwa na idara mbalimbali za matibabu
ikiwemo wadi ya watoto, Magonjwa ya kinamama, upasuaji wa moyo na mengine mengi.
Aidha, itakuwa na vifaa vya kisasa vya matibabu, ghorofa saba kwa ajili ya maegesho ya magari na vivuko 600. Pia kutakuwa na vitanda na wodi maalumu ya kutibia bure wale wasio weza kulipia huduma za Hospitali.
Kuanzishwa kwa Hospitali hiyo ni changamoto kwa waislamu wa nchi zingine ikiwemo Tanzania, ambapo kwa muda mrefu waislamu wamekosa Hospitali zenye kuzingatia adabu na nidhamu za kiislamu.
Nini maoni yako kuhusiana na taarifa hiyo? usisite kutuandkia maoni yako.