Monday, 5 December 2016

SHEREHE ZA MAULID MASJID MUZDALIFAH MIKOCHENI, USTAADH MUHAMMAD KHAMIS 'AMPIGA' USTAADH KOBA

SHEREHE za maulid ya kumswalia Mtume Muhammad jana zimefanyika katika msikiti wa Muzdalifah uliopo Mikocheni jijini Dar es salaam.
Sherehe hizo ambazo hufanyika kila mwaka msikitini hapo huanza baada ya kuswalia swala ya Ishaa mpaka saa tano usiku, huwashirikisha wasomaji Qaswida wawili mahiri na mashuhuri nchini, Ustaadh Muhammad Khamis na Ustaadh Ramadhani Koba. 

Wasomaji hawa huonesha umahiri wa kusoma Qaswida bila ya kutumia Dufu wakishirikiana na madrasa zao. Madrasa Siraj Munira kwa upande Ustaadh Koba na Madrasa Muzdalifa kwa upande Ustaadh Muhammad Khamis. 

Wasomaji hao huonesha umahiri wa kumsifu Mtume kwa naghma na njia mbalimbali za sauti. 
Katika shughuli ya jana Ustaadh muhammad Khamis ndiye aliyeng'ara zaidi kwa Qaswida yake ambapo iliwafanya wahudhuriaji kushindwa kujizua na kupelekea kumtunza pesa na kumsindikiza na mashairi.

Huu ni mfululizo kwa Ustaadh Muhammad Khamis kung'ara zaidi ya mwenzake katika shughuli hiyo inayoandaliwa na kudhaminiwa na Alhaj Aziz Rashid Mfaume maarufu kama Zingizi.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na masheikh wengi wakiwemo Sheikh Alhad Omar, Sheikh Hamid Jongo, Sheikh Mziwanda, Sheikh Waleed Alhad na Sheikh Uwesu kibosha.
Wengine ni Sheikh Hamis Mataka, Sheikh Ramadhani Abbas, Sheikh Yusuf Kidago, Sheikh Mahmoud Hussein Shadhly, Sheikh Zubeir Yahya na wengine wengi.

Shughuli ilifunguliwa kwa kusomwa Qurani na Ustaadh Hassani mtulia na mawaidha yalitolewa na Sheikh Othmani Maalim na Sheikh Othmani Khamis.

Msemo wa watu wa Qaswida, 'anayepigwa' katika shughuli ya Masjid Muzdalifah ni kwamba kapigwa mwaka mzima.