Tuesday, 1 November 2016

WAISLAMU WAFANYA MKUTANO KUJADILI MAKUNDI YA CHUKI DHIDI YA UISLAMU NCHINI AUSTRALIA

Waislamu wa Australia wamefanya mkutano msikitini kama mojawapo ya hatua za kupambana na chuki dhidi ya Uislamu.

Mkutano huo maalum uliandaliwa kwa ajili ya wageni wanaozuru Australia katika msikiti mmoja ulioko mjini Sydney ili kujadili mapambano ya makundi ya chuki dhidi ya Uislamu.
Wananchi wa Australia walipata fursa ya kuzuru msikiti huo wa Redfern uliojengwa na muungano wa jamii ya Kituruki.

Wageni waliozuru msikiti huo walivutiwa na kuridhishwa mno kwa fursa hiyo ya kuweza kuutambua Uislamu vyema.

Wageni hao pia walibainisha kujifunza mambo mengi kuhusu Uislamu na utofauti uliopo kati ya dini hii na dini nyinginezo.

Imamu wa msikiti Abdulrahman Şahin alitoa maelezo kuhusu mkutano huo.

Katika maelezo yake, Şahin alisisitiza umuhimu wa kuuelezea Uislamu kwa vitendo hasa kwenye nchi zisizotambua dini hii.

Mikutano kama hiyo ya kusaidia kupambana na makundi ya chuki dhidi ya Uislamu pia inaandaliwa katika misikiti mengine mbalimbali nchini humo.