Tuesday, 18 October 2016

SHERIA YA MARUFUKU KUVAA BURQA, NIQABU YAPINGWA NCHINI BULGARIA

UAMUZI wa Bunge la nchi ya Bulgaria la kupiga marufuku uvaaji wa Burqa na Niqabu kwa wanawake wa kiislamu katika maeneo ya umma kumepingwa vikali na makundi ya haki za binaadamu kwa kukiuka haki na uhuru wa dini.
Mkurugenzi wa Amnesty International Ulaya, John Dalhuisen anapinga kufuatia pendekezo la sheria mpya ya kuweka marufuku ya Burqa na Niqabu lililowekwa Septemba 30 mwaka huu.

"Wanawake nchi Bulgaria wanapaswa kuwa huru kuvaa Burqa au Niqabu kama sehemu ya utambulisho au
mafundisho ya dini yao yanavyowataka", alisema John Dalhuisen.

Kwa mujibu wa sheria hiyo ni marufuku kuvaa Burqa au Niqabu katika ofisi za serikali, Shule, taasisi za utamaduni na maeneo ya umma isipokuwa kwa sababu za Kiafya au maalumu.

Sheria hiyo inaiga nchi za Ufaransa, Uholanzi, na Ubelgiji ambazo zimepiga marufuku kwa wanawake wa kiislamu kuvaa Burqa na Niqabu katika maeneo ya umma.

Kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo atapigwa faini ya dola 114 mpaka 857. Nchi ya Bulgaria inakadiriwa kuwa na waislamu wanaofikia asilimia 12 ya idadi ya watu milioni 7.2.