WAISLAMU wameonywa dhidi ya kushiriki anasa wakati wa matukio ya kushtusha kama ya jua kupatwa.
Akiongea Alhamisi katika msikiti wa Jamia jijini Nairobi baada ya sala maalumu inayosaliwa na Waislamu jua linapopatwa (Kusuf) Imamu Mohamed Swalihu alisema watu wanatakiwa wamuogope Mungu zaidi anapozidi kudhihirisha uwezo wake kupitia matukio kama hayo ya jua kupatwa.
“Dunia inatakiwa ifahamu kuwa haya si mambo ya kusherehekewa ambapo wenzetu wanaenda kutalii au kulewa jua linapopatwa. Inafaa tutambue anayetekeleza haya ni nani na anataka nini? Tuombe msamaha kwa Mungu, tuepuke ufisadi na tudumishe amani nchini,” alisema Sheikh Swalihu.
Sala hiyo ya Kusuf iliyosaliwa kwa nusu saa baada ya jua kupatwa ilikusudia kuomba dua na msamaha kwa Mungu.
Isitoshe, Waislamu hutakiwa kunyenyekea na kukithirisha ibada kama ishara ya kutambua uwezo wa Mungu kila matukio hayo yanapojiri.
Jua lilipatwa kwa muda mchache jijini Nairobi na kwingineko barani Afrika kama Tanzania, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Msumbiji na kisiwa cha Madagascar.
Kupatwa huko kunakoitwa ‘Annular Eclipse’ hujiri mwezi unapokuwa katikati ya jua na sayari ya Dunia.
Wanaolitizama jua hilo moja kwa moja huenda wakadhurika macho na miale yake. Hupendekezwa walitizame kutumia darubini, kamera au miwani spesheli.
Wataalamu wanakadiria kuwa jua litapatwa tena kwa mbali (Annular Eclipse) Februari 26, 2017 na kupatwa kikamilifu (Total Eclipse) Agosti 21, 2017.