Wednesday, 24 August 2016

MWANAMKE WA KIISLAMU APIGWA FAINI NA KUFUKUZWA KATIKA BEACH KWA KUVAA HIJABU UFARANSA

Mwanamke wa kiislamu amepigwa faini ya dola 38 za kimarekani pamoja na kufukuzwa katika ufukwe wa Nice nchini Ufaransa kwa 'kosa' la kuvaa mavazi ya kusitiri mwili wake wakati wa kuogelea na kujipumzisha katika fukwe hizo.
Mwanamke huyo pia alitishiwa kumwagiwa maji ya kuwasha endapo angekaidi agizo hilo mbele ya polisi wanne waliokuwa wamemzunguka.

Mwanamke mwingine wa kiislamu mwenye umri wa miaka 34 nae alipigwa faini na kufukuzwa katika fukwe za Cannes nchini humo kwa kosa la kuvaa Hijabu.
Anaesma alivamiwa na Askari wapatao watatu na kumlazimisha kuvua Hijabu mbele ya watoto wake na watu walioko fukweni hapo.

Alidai kwamba walikuwa na lengo la kumdhalilisha zaidi kuliko kufuata utaratibu wa haki na sheria. Ufaransa imepitisha marufuku ya kutovaa Hijabu katika fukwe za Bahari nchini humo.

Tajiri Rachid Nekkaz mzaliwa wa Villeneuve-Saint-Georges
mwenye asili ya Algeria amesema kwamba yeye atalipa kila faini atakayotozwa mwanamke wa kiislamu kwa 'kosa' la kuvaa Hijabu.


Aliiambia CNN kwamba, "Niliamua kulipia faini zote za wanawake wanaovaa burkini ili kuhakikisha uhuru wao wa kuvaa nguo hizi, na zaidi ya yote, kutimiza matakwa ya dini yao dhidi ya sheria hii kandamizi."