Tuesday, 16 August 2016

MWANAMKE MWISLAMU WA KWANZA ACHAGULIWA KUGOMBEA UBUNGE MINNESOTA, MAREKANI

Mwanamke Mwislamu Mmarekani, Ilhan Omar ameweka historia kwa kuchaguliwa kugombea kiti katika Bunge la Wilaya ya 60B jimbo la Minnesota nchini Marekani.

Akizungumza baada ya matokeo ya uchaguzi huo wa mchujo wa Agosti 6, Ilan Omar wa chama cha Democrat na mwenye asili ya Somalia alisema, "Leo tumeandika historia. Leo ni mwanzo wa mustakabali mpya wa wilaya yetu.”
Ilhan Omar mwenye umri wa miaka 33 alizaliwa Somalia kabla ya kukimbilia Marekani kutokana na vita katika nchi yake.

Alipokimbia Somalia awali aliishi kwa muda wa miaka minne katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya kabla ya kuelekea Marekani katika eneo lenye Wasomali wengi la Cedar-Riverside ambapo aliishi kwa miongo miwili na sasa ni mkurugenzi wa Jumuiya ya Kuwaleta Pamoja Wanawake.

Omar amemshukuru baba yake, mume na watoto wake pamoja na hayati babu yake kwa kumfundisha kuhusu demokrasia.

Mwezi Novembe Omar atachuana na Abdimali Askar wa chama cha Republican katika uchaguzi wa kuwakilisha eneo hilo katika bunge la kieneo.