Wednesday, 6 July 2016

MUFTI WA TANZANIA AISHAURI SERIKALI KUTORUHUSU NDOA ZA JINSIA MOJA NCHINI

Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir ameiasa na kuishauri serikali kupiga marufuku na kutorusuhu ndoa za jinsia moja nchini.

Mufti aliyazungumza hayo leo jioni katika baraza la Eid El Fitr lililofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
mufti sheikh Abubakar Zubeir akizungumza na Rais John Magufuli
Alisema yeye kama Mufti lazima alisemee na kuligusia jambo hilo ambalo linatishia ustawi wa maadili ya watanzania na kama atakosekanika mtu wa kulikemea basi jamii inaweza kuangamia kama walivyoangamia watu wa Nabii Luti.

Aidha aliwataka watanzania kuacha ufisadi, kutoa na kupokea rushwa kwani Mwenyezi Mungu amekataza mambo hayo.

Mufti aliyazungumza wakati akijianda kumkaribisha Mgeni Rasmi wa Baraza la Eid El Fitr Rais wa Tanzania Dr. John Magufuli.

Akizungumza katika salamu za Eid, Rais Magufuli amesema kitendo cha Bakwata kuwaunganisha waislamu wote katika Baraza la Eid el-Fitr kinafungua ukurasa mpya na ni hatua muhimu za kuimarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu wa makundi mbalimbali pamoja na watanzania wengine wasio waislamu.


Aidha Rais Magufuli alisema serikali itahakikisha mali zote za waislamu zinakuwa salama na kwamba wote waliodhulumu mali za waislamu wanazirejesha.