Wanawake waislamu nchini Rwanda, wapigwa marufuku wasijifunike nyuso zao kwa kuvaa Niqabu.
Hatua hiii imechukuliwa na jumuiya ya waislamu nchini humo iliyofikia uamuzi wa kupiga marufuku vazi hilo la Niqabu linalovaliwa na wanawake.
Jumuiya hiyo imesema marufuku hiyo inatokana na sababu za kiusalama kwa waislamu na vilevile warwanda.
''Hili vazi ni la kiislamu hata hivyo limeanza kutumika vibaya kwa madhumuni ya kudhuru usalama wa waislamu na vitendo vinavyokinzana na mafunzo ya dini ya Kiislamu,'' alisema sheikh Mussa Sindayigaya.
Aliongeza kusema kuwa, ''Jambo la pili ni usalama wa nchi. kwa sababu watu wanajificha na kutenda vitendo pasi na kutaka kuonekana. Tumeona fikira potofu tayari ikifuja na ndipo sasa tukachukua uamuzi huu kuzuia kuenea kwa uovu."
Wanawoiunga mkono kauli hiyo ya jumuiya ya waislam nchini Rwanda wanasema kuwa Niqabu ilikuwa imeanza kutumika kuficha maovu mengi katika jamii.
Aidha wanasema kuwa wanawake waislamu wanapaswa kuwajibika kwa kujiepusha na maovu ambayo sasa yameanza kuchipuka kwa kisingizio cha Niqab.
Kuna wengine walioghadhabishwa na uamuzi huo lakini hawakutaka kuzungumzia suala hilo wakisema wanahofia usalama wao.
Hapo nyuma kundi la waislam zaidi ya 17 lilishikwa na kufunguliwa mashtaka ya kusajili vijana wa kujiunga na kundi la Islamic State na pia kueneza itikadi za kundi hilo.
