Wednesday, 13 July 2016

FATWA YA HUKUMU YA NDOA KWA WENYE JINSIA MBILI 'KHUNTHA' YATOLEWA LAHORE, PAKISTAN

TAKRIBAN maulamaa 50 wa kitivo cha taasisi ya Kiislamu isiyojulikana sana ya Tanzeem Ittehad-i-Ummat wametoa fatwa inayotoa ruhusa ya kisheria ya kufunga ndoa na mtu mwenye jinsia mbili (Khuntha) katika mji wa Lahore nchini Pakistan.
Fatwa hiyo iliyotolewa Jumapili ya mwisho wa mwezi June, ilisema mtu mwenye jinsia mbili, akiwa na “muonekano wa kiume” anaweza kumuoa mwanamke au mtu mwingine mwenye jinsia mbili lakini akiwa na “muonekano wa kike”, na pia kinyume chake.

Hata hivyo, fatwa hiyo iliongeza kuwa, mtu mwenye jinsia mbili, ambaye amebeba sifa za kuwa na “muonekano wa jinsia zote” haruhusiwi kuoa/kuolewa na mtu wa jinsia yoyote.

Aidha, imeamuliwa kwamba kupoka mgawo wa mirathi kwa watu wenye jinsia mbili ni ukiukwaji wa sharia na kwamba, wazazi wanowanyima urithi watoto zao wenye jinsia mbili wanakaribisha “ghadhabu za Mwenyezi Mungu”.

Maulamaa hao wametaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya wazazi wa aina hiyo.

Fatwa hiyo pia imeangalia mtazamo hasi wa jamii dhidi ya watu wenye jinsia mbili. Imekwenda mbali kiasi cha kuita kuwa ni “haram” kwa kitendo chochote kinachokusudia “kuwanyanyapaa, kuwatusi au kuwabeza”.

Fatwa hiyo ilimalizia na suala la mazishi, ikifafanua kwamba taratibu zote za mazishi ya watu wenye jinsia mbili tofauti zitakuwa sawa na za Waislamu wengine wanawake au wanaume.

Maulamaa waliotoa fatwa hiyo kuhusu watu wa jinsia mbili tofauti ni Imran Hanfi, Pir Karamat Ali, Abu Bakr Awan, Masoodur Rehman, Tahir Tabassum Qadri, Khalil Yousafi, Gul Ateequi, Gulzar Naeemi, Intikhab Noori, Abdul Sattar Saeedi na Khizarul Islam.