Mwislamu mmoja mkazi wa mji wa New York Marekani ameanzisha kampeni ya kutuma Aya za Qur'ani Tukufu kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Twitter katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu wametakiwa watume aya za Qur'ani katika mtandao wa kijamii wa Twitter katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Wanaotaka kushiriki katika kampeni hio watatumia hashtag ya #ttQuran kutuma aya fupi za Qur'ani Tukufu ili wengine waweze kuzisoma na kutoa maoni yao.
Halikadhalika mwendeshaji kampeni hiyo ametoa wito kwa Waislamu kujitahidi kusoma walau Juzuu moja ya Qur'ani kila siku katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kisha kuchagua aya moja katika Juzuu hiyo na kuituma katika Twitter kwa lugha ya Kiingereza.
Aidha wanaotuma aya wameombwa wakiweza wataje sababu ya kuiteua ili kuweza kuwa na mjadala mzuri katika mtandao huo wa kijamii.
Kampeni hiyo mbali na kuhimiza usomaji sambamba na uzingatiaji aya za Qur'ani katika fursa inayojitokeza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, pia inaandaa mazingira ya walio katika Twitter kubalisha mawazo kuhusu aya hizo tukufu.
