Thursday, 26 May 2016

SAMOA YATAKA KUPIGA MARUFUKU UISLAMU

Kasisi Ma'auga Motu ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Samoa anaishinikiza serikali ya nchi hiyo kupiga marufuku Uislamu katika visiwa.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Tuilaepa Sailele Malielegaoi wiki iliyopita alitoa wito wa kufanyiwa marekebisho vipengele vya uhuru wa kuabudu katika Katiba ya Samoa.

Alisema analenga kuhakikisha itikadi za Kikristo zinaingizwa kikamilifu katika katiba hiyo.
Kwa msingi huo Kasisi Motu amemtaka waziri mkuu kusonga mbele zaidi na kuupiga marufuku Uislamu ambao amedai ni tishio kwa mustakabali ya nchi hiyo.

Amebainisha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka idadi ya watu wanaovutiwa na Uislamu nchini humo na hivyo kuwafanya Waislamu wawe na ushawishi.

Katika kujibu matamshi hayo ya chuki dhidi ya Uislamu, Imamu Mkuu wa Samoa amesema Wakristo katika kisiwa hicho wanapaswa kuvumilia dini nyinginezo na kuacha vitendo vya ubaguzi.

Imam Mohammad bin Yahya amesema Samoa inaweza kupata matatizo ya kufanya biashara na nchi za Kiislamu iwapo katiba ya nchi hiyo itabadilishwa. 

Katika sense ya mwaka 2001, ilibainika kuwa asilimia 0.03 ya wakaazi wote wa visiwa ni Waislamu huku walio wengi wakiwa ni Wakristo.

Samoa ni nchi iliyo katika Bahari ya Pasifiki inayojumuisha visiwa viwili vikuu vya Savai'i na Upolu na visiwa vingine vidogo. samoa iliyo kati ya Hawai'i na New Zealand mji wake mkuu ni Apia huku ikiwa na idadi ya watu wake ikikadiriwa kuwa 190,000.