katika sherehe za Jumanne Usiku za kuwaenzi washindi wa Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran yaliyofanyika Tehran, baada ya washindi katika vitendo vya hifdh na Qiraa kupata zawadi, Msomaji (Qari) wa Tanzania Ustaadh Rajai Ayoub ameenziwa kutokana na kuwa na sauti na lahni bora zaidi miongoni mwa washiriki wote kutoka zaidi ya nchi 70 duniani.
Ustaadh Rajai amepewa cheti maalumu kama msomaji mwenye sauti nzuri kuliko wote katika Mashindano hayo.
Hii ni mara ya kwanza kutolewa kwa cheti hicho na Rajai anakuwa mtu wa kwanza kupokea cheti hicho.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na miongoni mwa washiriki kutoka nchi zingine walisema Qarii Mtanzania alikuwa na Saudi bora zaidi.
Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalizinduliwa rasmi Jumatano iliyopita na kumalizika jana Jumanne katika Ukumbi Mkubwa wa Sala wa Imam Khomeini MA mjini Tehran.
Nchi zaidi ya 70 zilituma wawakilishi katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ambayo yalikuwa na washiriki 130.
Kaulimbiu ya mashindano ya mwaka huu ilikuwa ni "Kitabu Kimoja Umma Moja”.

