Saturday, 16 April 2016

PAPA ACHUKUA WAHAMIAJI 12 WA KIISLAMU WA SYRIA KUTOKA LESBOS KWENDA NAO VATICAN

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewachukua wahamiaji waislamu 12 kutoka Syria na kwenda nao Vatican baada yake kutembelea wahamiaji katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki.

Wahamiaji hao kutoka familia tatu wote ni Waislamu, na miongoni mwao kuna watoto sita.

Nyumba za familia hizo zilishambuliwa kwa mabomu wakati wa vita nchini Syria.

Vatican imesema kupitia taarifa kwamba Papa Francis amechukua hatua hiyo kuwaonesha wahamiaji kwamba wanakaribishwa.
Maelfu ya wahamiaji kwa sasa wamekwama katika kisiwa cha Lesbos kufuatia mkataba wa mwezi jana kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ambao unalenga kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya.

Wahamiaji wote walioondoka na Papa walikuwa tayari wanaishi Lesbos kabla ya mkataba huo kuanza kutekelezwa, Vatican imesema.

Chini ya mwafaka huo baina ya EU na Uturuki, wahamiaji wanaofika kwa njia haramu katika visiwa vya Ugiriki kutoka Uturuki baada ya tarehe 20 Machi watakuwa wakirejeshwa Uturuki iwapo hawatafanikiwa kuomba hifadhi.