Mwenyezi Mungu ametubainishia wazi katika aya za Quran tukufu kuwa amemtuma mtume Muhammad ﷺ ulimwenguni kuwa kama mjumbe, mwonyanji, na mwongozaji wa njia iliyonyooka. Mtume wetu ni mfano wa mwanga ulioletwa kuja kumulika dunia na kutuongoza.
Mtume wetu Muhammadﷺ aliyetumwa kwetu ameweza kuishi kwa kuzingatia maamrisho ya dini aliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Aliweza kutekeleza masharti yote ya dini pasi na kuacha hata chembe kama alivyousiwa na Mwenyezi Mungu. Kufuatia mfumo wake wa maisha, mtume wetu Muhammadﷺ ameweza kuwa mfano bora kwa jamii ya Waislamu na kuwakilisha dini ya Kiislamu kwa ujumla.
Dini ya Kiislamu imeletwa kwetu kikamilifu na kwa mifano bora kupitia mtume Muhammadﷺ ambaye ana umuhimu mkubwa.
Yeye ni mtume aliyeishi kwenye jamii iliyokuwa imepotoka kwa ushirikina, ukafiri, na dhuluma na akaweza kuibadilisha na kuiweka kuwa katika mfumo wa maadili ya Kiislamu. Uwezo huo wa kuibadili umma huo unaweza kusemekana kuwa pia miujiza mengine baada ya Quran.
Katika Quran tukufu, kuna aya inayompa sifa mtume Muhammadﷺ kwa unyenyekevu wake na kumuweka katika wadhifa mkuu. Kuna baadhi ya hadithi pia zinazozungumzia suala hili na kudhihirisha umuhimu wake mkubwa katika dini ya Kiislamu.
Mtume Muhammadﷺ amewekwa katika daraja ya juu kutokana na hulka na mienendo yake iliyomfanya kuweza kuaminika.
Yeye alikuwa akitimiza ahadi zote anazotoa kwa wakati unaotakiwa. Hakuwezi kukengeuka kitabia wala kupoteza uaminifu aliokuwa nao. Hakuweza kusema uongo hata kwa dhihaka.
Hata aliweza kupewa jina la lakabu la “Muhammad ul-Amin" na jamii aliyokuwa akiishi nayo kabla ya kupewa utume kutokana na sifa yake ya uaminifu aliyokuwa nayo.
Watu wasiokuwa waumini pia waliweza kumuamini na hawakuwahi kumdanganya.
Mtume Muhammadﷺ amewataka watu wote kuwa na uaminifu na kusema ukweli daima bila ya kutia uongo hata chembe. Hizi ni baadhi ya sifa zinazoweza kumpelekea mwanadamu peponi.
Mtume Muhammadﷺ amekuwa mfano bora kwa Waislamu kutokana na hulka yake, tabia yake, huruma, unyenyekevu, mwenye kutabasamu na mpole.
Hakuwa na moyo wa chuki wala roho mbaya. Kinywa chake hakikuwahi kutoa maneno wala kauli chafu inayoweza kuvunja mtu moyo. Hakuwahi kutoa aibu ya mtu mbele ya hadhira bali alikuwa mpole mwenye utulivu na subira.
Alikuwa akiwasamehe wanaomkosea na hakuwekea mtu yeyote chuki wala husuda. Kila alipoalikwa, alijitahidi kadri ya uwezo wake ili kuhudhuria. Hakuvunja mtu moyo na alihimiza usawa katika jamii pasi na kuzingatia utofauti wa utajiri au umasikini, ukuu au utumwa, ukubwa au udogo. Alihimiza misaada kwa watu maskini, kutembelea wagonjwa na kutazama mayatima.
Anas bin Malik swahaba ambaye alimhudumia mtume Muhammadﷺ tangu alipokuwa na umri wa miaka 10, pia amemsifia kwa kusema kwamba hakuwahi kumsikia akimkemea wala kumkasirikia kwa jambo lolote katika maisha yake.
Mtume Muhammadﷺ pia ameweza kutoa mafunzo ya utekelezaji wa ibada za Mwenyezi Mungu kwa umma wake wa Kiislamu. Amesisitiza umuhimu wa kutekeleza ibada hizo mara kwa mara pasi na mapungufu.
Ameweza kutukumbusha kuwa wanadamu wameumbwa kwa lengo la kumuadubu Mwenyezi Mungu pekee. Vile vile ametuusia kuwa ibada na matendo mema ya misingi ya kidini ndiyo inayoimarisha imani ya mwanadamu.
Mtume Muhammadﷺ pia ameweza kutupigania ili kurahisishiwa ibada na Mwenyezi Mungu. Kwa mfano, tumeweza kuruhusiwa kufupisha ibada za swala hasa wanapokuwepo watoto, kina mama na wazee katika safu za maamuma.
Umuhimu mwengine mkubwa wa mtume Muhammadﷺ kwetu sisi Waislamu ni dua alizoomba kutokana na huruma aliyokuwa nayo kwa lengo la kutufanya tuwe umma bora katika siku ya Qiyama.
Kuhusiana na suala hili, mtume wetu Muhammadﷺ anasema maneno haya; “Kila mtume anayo dua yake maalum kwa ajili ya umma wake. Mimi pia ninayo dua yangu niliyoiweka hadi siku ya Qiyama kwa ajili ya umma wangu."
Kutokana na kauli hii, wasomi wote wa Kiislamu wametoa ufafanuzi unaosema kwamba jumuiya nzima ya Waislamu itaweza kuokolewa na mtume Muhammadﷺ siku ya Qiyama baada ya Mwenyezi Mungu kutoa hukumu yake.
