BABA Muingereza amepigwa marufuku kumpeleka mwanawe wa kiume kanisani baada ya mama wa mtoto huyo ambaye ni Muislamu kushinda kesi baina yao iliyokuwa ikinguruma kwa muda mrefu.
Baba huyo asiyefuata misingi ya Uislamu na ambaye ana ushirikiano wa karibu na jamii ya Wakristo, na ambaye pia ametalikiana na mama wa mtoto, ameonywa kwamba anaweza kunyimwa fursa ya kukutana na mtoto wake huyo mwenye miaka tisa ikiwa atajaribu kumpeleka kanisani.
Na sasa baba huyo, aliyezaliwa Uingereza kwa wazazi wenye asili ya Pakistani, anapinga uamuzi uliotolewa awali na Jaji Williscroft wa Mahakama ya Wilaya ya Derby County mwanzoni mwa mwezi huu.
Wiki iliyopita, baba huyo alikata rufaa Mahakama Kuu akitaka uamuzi huo wa mahakama ya Wilaya utenguliwe.
"Jaji huyu anaogopa tu kuambiwa kuwa anauchukia Uislamu," alisema na kuongeza kuwa, "Nataka mwanangu awe na maisha ya kati kwa kati ambayo yanamuwezesha kupata nafasi ya kusikiliza Imani tofauti na mwishowe kufanya uamuzi wake, kama atakuwa nao, kuhusiana na dini ipi ya kufuata."
Baba huyo, ambaye hawezi kutajwa jina lake kwa sababu za kisheria, alisema mtalaka wake alisisitiza kuwa mtoto wao huyo wa kiume, ambaye hivi sasa anamlea katika makuzi ya Kiislamu, anaweza ‘kuchanganywa’ ikiwa atapata mafundisho ya dini nyingine.
"Mtoto wangu amekuwa akipewa mafundisho ya aina moja na namna pekee ninayoweza kumuonyesha vitu vingine ni kumpeleka katika maeneo tofauti," alisema baba huyo.
“Kama sitamuonyesha aina nyingine za maisha atakuwa kama kondoo bubu. Nataka aone na kujifunza tamaduni tofauti.
“Huku ni kumharibu kifikra. Tayari ameshaanza kuniambia kuwa nina moyo uliokufa, kwamba mimi ni mtu mbaya, kwa sababu sifuati maadili ya Kiislamu. Najisikia vibaya kuona kwamba ninalazimika kumuweka mbali na harakati za watoto wengine kwenye jamii yetu.
"Amekuwa akilishwa uongo uleule niliopewa mimi wakati nikiwa mtoto na sasa ninamtakia yeye mema. Jaji huyu aliegemea zaidi kuangalia kwa jicho la kisiasa kuwa hakosei na hivyo akapuuza ushawishi wangu kama baba mpendwa. Naogopa kwamba ataacha kuniona kwa sababu ya mafunzo anayopata."
Mwanaume huyo na mtalaka wake walioana mwaka 2003 na (mwanaume) aliendesha aina ya maisha ya Kimagharibi.
'Hilo lilikuwa muhimu kwangu kwa sababu ya sheria kali za kidini ambazo nimekulia,' alisema.
'Nilifundishwa kwamba Wakristo ni katili na hawana maadili, kwamba ni Waislamu tu ndiyo wenye dini ya Amani na nyingne zote ni za kishetani. Ni hadi pale nilipoanza kujichanganya na Wakristo ndipo nilipobaini kwamba mafunzo hayo niliyopewa hayakuwa na maana.'
Lakini mkewe aliyezaliwa Pakistani aligeukia maisha ya Uislamu baada ya kifo cha baba yake mwaka 2007, wakati mama yake alipomwambia kwamba, kwa sababu (baba yake) hakufuata misingi ya dini yake (Uislamu) atakwenda jehanamu, na atabaki huko milele mpaka pale yeye (mke) atakapokuwa Muislamu mchamungu.
Kuanzia hapo, mwanamke huyo alianza kuhudhuria madrasa kituo cha kutolea mafunzo ya Kiislamu akivaa hijab na kuachana na marafiki Wakristo.
Aliachana na mumewe mwaka 2013, akimchukua pia mtoto wao wa kiume. Wanandoa hao waliachana mwaka jana baada ya mwanaume huyo kuanza kufuata Ukristo.
Mtoto huyo anaishi na mama yake lakini humuona baba yake kila mwishoni mwa wiki.
“Baada ya talaka, jamii ya Kikristo ilinipokea,” mwanaume huyo alisema.
"Wanafanya vitu vingi ambavyo mwanangu huvipenda na hivyo huwa naenda kanisani na ninataka kumpeleka.
Lakini mama yake alipojua, akashitaki mahakamani na kupata pingamizi ambalo linamzuia mtoto wangu kwenda kwenye jambo lolote la Wakristo."
Amri hiyo inamzuia baba kumpeleka mtoto wake katika tukio lolote la dini. Anaagizwa kwamba ni lazima ampatie chakula halali na kuhakikisha kuwa mtoto anakuwa ‘Muislamu wa kawaida na kufuata sharia za Kiislamu'.

