Wafungwa 10 wenye asili ya Yemen ambao wamekuwa wakizuiliwa katika jela ya kijeshi ya Guantanamo Bay siku ya Alhamis wamesafirishwa hadi Omani hatua ambayo ni mojawapo ya malengo ya rais Barack Obama ya kufunga kituo hicho kabla ya kuondoka madarakani.
Uhamisho huo wa wafungwa hao kutoka kwa kituo cha mahabusu wa kimataifa ni hatua ambayo inaleta nuru ya kufungwa kwa kituo ambacho kimekuwa kikilaaniwa kimataifa.
Rais Barack Obama amekuwa na azimio la kufunga jela hiyo tangu alipokuwa rais mnamo mwaka 2009.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wafungwa hao 10 kutoka Yemen walizuiliwa katika jela hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja bila ya kushtakiwa wala kuhukumiwa.
Obama ambaye anatarajiwa kuondoka ofisini mnamo mwezi Januari mwaka 2017,amekuwa akishinikiza kufungwa kwa jela hiyo ila anapata upinzani mkuu kutoka kwa mashirika mbalimbali.
Afisa mmoja wa ngazi za juu Omani alifahamisha kuwa wafungwa hao tayari wamewasili nchini na wataendelea kukaa hapo kwa sababu za kiusalama hadi pale hali ya Yemen itakapokuwa sawa na salama.
Duru zaarifu kuwa kwa sasa takriban wafungwa 93 wa kimataifa wamebaki katika jela hiyo ya kijeshi ya Guantanamo Bay.
