Wednesday, 23 December 2015

WAISLAMU WAWAKINGA WAKRISTO KUULIWA NDANI YA BASI NA AL-SHABAB

Watu wawili wameuliwa na wanamgambo wa Al shabbab huku abiria wa kiislamu waliokuwa ndani ya basi wakiwakinga wenzao wa kikristo kuuliwa na kundi hilo ndani ya basi huko Mandera. 

Waziri wa usalama wa ndani Jospeh Nkaissery amesema abiria wa kiislamu wamekataa kutenganishwa na wakristo baada ya kutambua kuwa jamaa hao walitaka kuwauwa wakristo. 

Nkaissery amekisifu kitendo hicho cha waislamu akisema kimetoa taswira nzuri ya umoja wa wakenya licha ya imani zao tofauti. 
Kulingana na jamaa aliyeshuhudia tukio hilo ni kuwa wanamgambo hao walilimiminia risasi basi hilo la kampuni ya Makkah na kuua abiria mmoja huku mwengine akiuliwa kwenye lori.

Gavana wa Mandera Ali Roba ambaye ameshutumu tukio hilo, amesema kuwa wenyeji wa eneo hilo waliokuwa wakisafiri katika basi hilo, walipinga hatua hiyo na kuwataka magaidi hao wawaue wote bila kuwatenganisha jambo lililowapelekea magaidi hao kuingiwa na hofu ya kukabiliwa na kutoroka.

Aidha mratibu wa kaskazini mashariki mwa eneo hilo Mohmoud Saleh amesema ingawa dereva wa basi amejeruhiwa hakusimamisha basi hilo wakati wa shambulizi hilo hadi kufika eneo la Dabacity.

Kulingana na Naibu wa kamishna wa eneo hilo Julius Otieno, tukio hilo lilitokea kati ya eneo la Dabacity na Borehole II.

Kulingana na ripoti ya kitengo cha ujasusi nchini kupitia kwa wenyeji, zaidi ya wanamgambo mia mbili wa Al-Shabab wameingia nchini katika eneo la Kotolu kutoka Somalia katika kipindi cha wiki tatu.

Naye gavana wa ManderaAli Roba ambaye ameiandikia wizara ya usalama wa ndani taarifa hio, ametaka wanajeshi kufanya msako kwa miguu badala ya kutumia magari ili wawafurushe wanamgambo hao kutoka eneo hilo.