Waziri Mkuu wa Somalia, Abdiweli Sheikh Ahmed, Jumanne wiki hii amewatolea wito kundi la Al-Shabaab kuachana na ghasia na kukiri kwamba wameshindwa kufuatia mkutano wake na Baraza la Usalama la Taifa mjini Mogadishu.
Rais Hassan Sheikh Mohamud alisimamia kikao hicho, ambapo maafisa wa ngazi za juu serikalini, usalama na jeshini walijadiliana kampeni ya kijeshi inayoendelea dhidi ya Al-Shabaab na mipango ya serikali kurejesha utulivu kwenye maeneo yaliyokombolea hivi karibuni.
"Hatutasitisha operesheni zetu hadi Somalia na Wasomali wote wawe huru dhidi ya kitisho na ukandamizaji wa Al-Shabaab," alisema Ahmed. "Tunashinda vita hivi na sasa ni wakati wa al-Shabaab kuachana na mapigano."
Ahmed aliiomba jamii ya kimataifa kusaidia jitihada za serikali kutoa msaada wa chakula kwa watu walio kwenye hali ngumu katika maeneo yaliyokombolewa.
