Sunday, 16 March 2014

WAUMINI WAKATAA KUMZIKA KIONGOZI WAO WAKIDAI ATAFUFUKA, WAAMINI HAJAFA YUPO KATIKA TAFAKARI

Guru wa India Ashutosh Maharaj aliyeaga dunia amekuwa akihifadhiwa katika barafu kwa karibu majuma sita, huku wafuasi wake wakiwa na imani kwamba atafufuka na kuendelea kuwaongoza, msemaji wake amesema.

Wafuasi walimweka Ashutosh Maharaj katika barafu, na wamekuwa wakilinda mwili wake katika ashram, kwenye mji mdogo uliopo jimbo la Punjab.

Ashutosh Maharaj ambaye alitangazwa kufariki Januari 29 mwaka huu, aliripotiwa kuwa na umri usiopungua miaka 70, na ni mmoja wapo wa maguru wengi wa India ama watu wenye imani kuu ambao waliongoza Divya Jyoti Jagrati Sansthan (Divine Light Awakening Mission) na linadai kuwa na mamilioni ya wafuasi kote ulimwenguni.

Msemaji wa kundi hilo Swami Vishalanand alisisitiza kuwa kiongozi wao hajafariki lakini alikuwa katika hali ya mawazo, na kwa hivyo angali  hai.

Vishalanand alisema kuwa sasa wafuasi wake wanamsubiri amalize hali hiyo ya kutafakari. Hadi hilo litakapofanyika, ashram iliyopo mji wa Nurmahak itaendelea kuwa wazi wafuasi wakiendelea tafakari zao na vipindi vya dini.

“Mahara-ji bado anatuma jumbe kupitia kwa wafuasi wanaotafakari kulinda mwili wake hadi atakaporudi tena,” alisema.

Uamuzi wa kuweka mwili katika barafu ulipingwa mahakamani na mtu anayedai kuwa dereva wake wa zamani, ambaye alidai kuwa wafuasi kadha hawauachi mwili huo kwa sababu wanataka sehemu ya mali ya guru huyo, vyombo vya habari viliripoti.

Lakini mahakama ilikataa kesi ya mtu huyo baada ya kupokea habari kutoka kwa wakuu husika ya kuthibitisha kifo chake kilichotokana na mshtuko wa moyo, alisema Reeta Kohli, wakili katika jimbo la Punjab.

“Mahakama ilikataa maombi yake baada ya serikali ya Punjab kusema kuwa mtu huyo amefariki na kwamba ni uamuzio wa wafuasi wake kuamua kile wanachotaka kufanya na mwili wake,” alieleza Kohli.

Afisa wa polisi wa ngazi za juu Gurinder Singh Dhillon alisema polisi “hawawezi kuingilia kati” sasa kwa vile mahakama imefanya uamuzi wake.

Mtandao wa Maharaj ambao unasema kuwa kundi hilo lilianzishwa 1983 na lina vituo vya kiroho kote ulimwenguni, limewashukuru wafuasi wake kwa kusimama pamoja nalo huku guru wake akiendelea na tafakari yake.

Vishalanand alisema kuwa viongozi wengi wa kidini katika historia wamekuwa wakisafiri Himalayas kwa miezi mingi kukiwa na baridi kali, kabla ya kupata tena uhai.

Msemaji mwingine, ambaye anaongoza kijiji cha karibu na hapo ambapo wafuasi wengi wa Maharaj wanaishi, alisema kuwa wao watasubiri tu.

“Tunapofunga macho yetu, tunaweza kuzungumza na Maharaj, ambaye ametuhakikishia kuwa atarudi,” Lakhwinder Singh  aliambia gazeti la Indian Express.


Ashutosh Maharaj