Klabu hiyo iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya Anelka kutangaza kupitia mtandao wa kijamii kuwa anaacha kazi.
Anelka alisema kuwa anaondoka katika klabu hiyo baada ya kukosa kutatua tofauti zilizopo kati yake na timu hiyo kuhusu ishara yake yenye utata ambayo inasemekana kuwa ya kibaguzi dhidi ya wayahudi.
Mshambuluaji huyo mwenye umri wa miaka 35, alipigwa marufuku kutocheza mechi tano na kutozwa faini ya pauni 80,000 na shirikisho la soka Uingereza, kwa kufanya ishara hiyo, baada ya kufunga bao dhidi ya klabu ya West Ham mwezi Disemba mwaka jana.
West Brom imechukua hatua ya kumfuta kazi Anelka kutokana na ishara hiyo na pia kwa sababu ya matamshi yake kwenye mtandao wa kijamii.
Awali aliachishwa kazi mwa muda na Albion, wakati klabu hiyo ilipokuwa inafanya uchunguzi wake binafsi.
Mapema siku ya Ijumaa, Anelka alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaondoka katika klabu hiyo.
Aliandika kwamba, "kufuatia mazungumzo kati yangu na maafisa wa klabu, kuna masharti kadhaa ambayo wamenipa kabla ya kujiunga tena na klabu hiyo, Masharti ambayo siwezi kuyakubali''.
Hata hivyo klabu ilisema kuwa masharti yaliyotolewa kwa Anelka ni pamoja na kumtaka awaombe msahama mashabiki, wadhamini na jamii kwa ujumla kwa athari iliyotokana na ishara yake aliyoifanya Disemba tarehe 28 na pili akubali kutozwa faini.
Mwanzoni akizungumzia tukio hilo Anelka alisema alama yake haikuwa dhidi ya Wayahudi, kwamba ni ishara kwa rafiki yake mchekeshaji (comedian) wa kifaransa Dieudonné M'bala M'bala.
"Hii ishara ilikuwa ni maalum kwa rafiki yangu Dieudonne," aliandika Anelka katika akaunti yake ya twitter kwa lugha mbili ya kiingereza na kifaransa.
"Nawaomba watu wasitiwe ujinga na vyombo vya habari, mimi si mbaguzi wa rangi wala kwa wayahudi", alisisitiza
Anelka alisilimu mwaka 2004 huko katika nchi ya Falme za kiarabu na kutumia jina la Abdul-Salam Bilal.
![]() |
Kushoto ni mchekeshaji Diedonne M'bala M'bala na kulia ni Anelka wakionesha ishara inayotafsiriwa kama ubaguzi kwa wayahudi |