Sunday, 23 March 2014

WABUNGE WANAWAKE WAMTAKA RAIS KENYATA AKATAE MSWADA WA WANAUME KUOA WAKE WENGI

WABUNGE wanawake wamemrai Rais Uhuru Kenyatta asiidhinishe mswada wa ndoa ambao ulipitishwa Bungeni Alhamisi usiku wakisema kipengee kinachoruhusu ndoa ya wake wengi kinadunisha nafasi wa mke katika familia.

Aidha, pendekezo kwamba yeyote atakayevunja ahadi ya ndoa ataadhibiwa liliondolewa, baada ya wabunge wanaume kudai kuwa itatumiwa vibaya na kina dada kudai ridhaa kwa njia ya udanganyifu.

Wabunge hao wanawake Alhamisi jioni walimtaka Rais kuurejesha mswada huo bungeni ili kipengee kinachomruhusu mume kuwaoa wake zaidi ya moja bila kushauriana na mke wa kwanza kiondolewe, wakisema kitapelekea ongezeko la misukosuko na hata kusambaratika kwa asasi ya familia.

“Wanaume wakiruhusiwa kuwaoa wanawake wengine bila kuwajulisha wake zao familia zitasambaratika na watakaoumia na watoto ambao wana haki ya kupata malezi bora chini ya familia thabiti. Bunge halifai kuunda sheria ambayo itapelekea kuvunjika kwa ndoa nyingi humu nchini,” akasema Mbunge wa Kilome Bi Regina Muia.

“Hii ndio maana sisi kama wabunge wanawake tunamhimiza Rais kutotia saini mswada huu ambao ni hatari kwa  uthabiti katika familia,” aliongeza.

Bi Muia na Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Garissa Bi Shukran Gurre waliwaongoza wenzao kuondoka bungeni kwa hasira pale wenzao wanaume  walipoungana kuipitisha marekebisho ya kifungu cha 44 cha mswada huo ili kuwaruhusu wanaume kuoa wanawake wengine bila kuwajuza wake wao wa kwanza.

Wengine walikuwa; Ann Gatecha Nyokabi (Kaunti ya Kiambu) na Grace Kiptui (Baringo).

Hata hivyo, idadi ya wanawake waliokuwa Bunge ilikuwa ndogo ikilinganishwa na wezao wanaume. Bunge la Kitaifa lina wanawake 16 waliochaguliwa, 4 wateule na wawakilishi wa wanawake wanaowakilisha kaunti 47 nchini.

Marekebisho hayo yaliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Sheria Bw Samuel Chepkonga (mbunge wa Ainapkoi, URP)  na kuungwa mkono na wabunge wanaume.


Makamu mwenyekeiti wa wabunge wanawake nchini Kenya Zeinab Chidzuga