Saturday, 22 March 2014

ANT BALAKA WADAI WAKO TAYARI KULETA AMANI JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Wanamgambo wa Kikristo wa Anti Balaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wametangaza kuwa wako tayari kurejesha umoja wa kitaifa nchini humo.

Hayo yamesemwa na Antoinette Montaigne Moussa, Waziri wa Mawasiliano na Umoja wa Kitaifa wa nchi hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa wanamgambo hao wenye misimamo mikali. 

Kwenye mazungumzo hayo, Emotion Brice Namsio Msemaji wa kundi la Kikristo la Anti Balaka amesema kuwa, kundi hilo liko tayari kuweka chini silaha zao na kufanya mapatano na Waislamu. 

Kundi hilo limedai kuwa, machafuko yanayoendelea nchini humo yanakinzana na malengo yao, na eti malengo yake ni kuwakomboa wananchi wa nchi hiyo. 

Naye Waziri wa Mawasiliano na Umoja wa Kitaifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameupokea vizuri uamuzi huo na kuongeza kwamba serikali ya Bangui ina matumaini kuwa msimamo wa kundi hilo hautabadilika.

Kuanzia mwezi Disemba mwaka 2013 kundi la Kikristo la Anti Balaka limekuwa likifanya mauaji ya kinyama na ya kutisha dhidi ya Waislamu nchini humo, na kusababisha maelfu ya waumini hao kulazimika kuyakimbia makazi yao.