Tuesday, 4 March 2014

SHEIKH PONDA ALALAMIKIA PINGAMIZI DHIDI YAKE, HATIMA YA KESI YAKE MARCHI 18

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itupilie mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na isikilize maombi yake ya mapitio ili haki itendeke.

Sheikh Ponda, ambaye kwa sasa yuko mahabusu kutokana na kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro ya kudaiwa kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro na kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wake, Juma Nassoro alitoa ombi hilo jana mbele ya Jaji Augustine Mwarija ambaye anatarajia kutoa uamuzi dhidi ya kesi hiyo Machi 18,2014.

Wakili Juma Nassoro alidai kuwa maombi ya mapitio yaliyopelekwa mahakamani hapo na Sheikh Ponda wakati kesi yake ikiendelea si jambo geni na kwamba yeye si wa kwanza kufanya hivyo.

Alitoa mifano ya kesi nyingi, ikiwamo kesi namba 14/2013 ya ugaidi ambayo ilikuwa ikimkabili Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph Lwezaura ambao walitoa changamoto ya kujua uhalali wa mashtaka ya ugaidi na mahakama ikaona kweli wana haki na ikawafutia.

Wakili huyo wa Ponda aliiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kukataa maombi yake ya kumfutia shtaka.

Kutokana na maombi hayo, DPP aliwasilisha pingamizi akiiomba mahakama iyatupilie mbali akidai yamewasilishwa kinyume cha sheria.

Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alidai maombi hayo yamekiuka kifungu cha 372 (2) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.