Thursday, 20 March 2014

SHEIKH PONDA AKATALIWA TENA OMBI LAKE MAHAKAMANI

Mahakama Kuu imetupilia mbali kwa mara ya pili ombi la marejeo lililowasilishwa na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda kwa sababu maombi hayo hayapo sahihi kisheria.

Sheikh Ponda kupitia kwa wakili wake, Juma Nassoro, aliwasilisha maombi ya marejeo, akiiomba Mahakama ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kukataa maombi yake ya kumfutia shtaka la kukaidi amri ya mahakama.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Agustine Mwarija, baada ya kupitia vifungu vya sheria na hoja zilizotolewa na upande wa Serikali na ule wa utetezi.

Jaji Mwarija alisema maombi yaliyowasilishwa na Sheikh Ponda kupitia wakili wake, Juma Nassoro, sheria ambayo wameitumia kuwasilisha maombi hayo hairuhusu maombi hayo kuletwa, isipokuwa amri iliyotolewa inamaliza kesi kwa kuwa amri hiyo inamaliza ilikuwa inamaliza kesi na si kesi ya msingi.

Baada ya kusema hayo, Jaji Mwarija alisema amekubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupitia Wakili Mkuu wa Serikali, Bernard Kongola.

Kongola alidai kuwa, ombi hilo liliwasilishwa kinyume na kifungu cha 372 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambapo aliomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo.

Jaji Mwarija alisema tafsiri iliyotolewa na mleta maombi (Sheikh Ponda), katika sheria hiyo si sahihi, kwa sababu haikuhusu maeneo kama yalivyoelezwa katika tafsiri za Mahakama ya Rufani, kutokana na tafsiri hiyo kuwa pana zaidi.

Alisema uamuzi uliotolewa awali, haukumaliza mashitaka yote kati ya mahstaka matatu, ambapo alisema kifungu hicho cha sheria hakihusu kumaliza shauri kutokana na shauri la awali, bali ni shtaka lote.

Hata hivyo, alisema Mahakama hiyo ina mamlaka ya kufanya mapitio kwa hiari yak echini ya kifungu namba 372 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Pia alisema kuhusu suala la kuwa kesi ya Ponda si ya kwanza kuwasilisha ombi hilo wakati kesi ikiendelea kama Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama (Chadema), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph waliwasilisha ombi la kupinga mashtaka ya ugaidi yanayowakabili wakati kesi ikiendelea.

Alisema kesi ya Lwakatare haikufanyiwa mapitio ya hoja yoyote, ambapo Lwakatare alikuwa akipinga kesi na kutaka kesi hiyo ifutwe.

Sheikh Ponda kwa sasa yuko mahabusu kutokana na kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, akidaiwa kufanya makosa ya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro na kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.