Polisi wa Uganda wameimarisha usalama baada ya kupokea habari za kijasusi kwamba wanamgambo wa Al-Shabab wanapanga kuishambulia malori yanayosafirisha mafuta.
Al-Shabab mara kwa mara imekuwa ikionya kwamba itaishambulia Uganda kwa sababu ina majeshi yake nchini Somalia kulinda usalama.
Wanamgambo wa Al-shabab waliishambulia Uganda mwaka wa 2010. Takriban watu 76 waliokuwa wamekusanyika kwenye uwanja wa Raga wa Kyadondo kutizama fainali za Kombe la Dunia waliyapoteza maisha yao baada ya mabomu mawili kulipuka.
Tokea wakati huo, kundi la Al-Shabab limekuwa likitishia kuzishambulia nchi zote ambazo zimeyatuma majeshi yake nchini Somalia kulinda usalama chini ya mwavuli wa Umoja wa Afrika. Uganda ndio iliyokuwa nchi ya kwanza kutuma majeshi mwaka wa 2007.
