Wawakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC katika Umoja wa Mataifa wamelaani hujuma za hivi karibuni za Wazayuni huko Baitul Muqqadas, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Imearifiwa kuwa mabalozi wa nchi wananchama wa OIC jana waliitisha kikao cha dharura katika Umoja wa Mataifa kujadili uchokozi wa hivi karibuni wa Utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palesitna katika Umoja wa Mataifa Riyadh Mansour amehutubia kikao hicho cha OIC na kutoa ripoti kuhusu vitendo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni dhidi ya mji wa Baitul Muqaddas na hasa Msikiti mtukufu wa Al Aqsa.
Afisa huyo wa Palestina ametoa wito kwa nchi za Kiislamu duniani kuchukua hatua dhidi ya hujuma na uchokozi wa utawala haramu wa Israel.
Mansour amesema kuwa vitendo vya Israel ni kinyume cha sheria za kimataifa. Amekumbusha kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imewasilisha malalamiko yake mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo ameitaka OIC nayo ichukue hatua sawa na hiyo.
