Wednesday, 19 March 2014

MUSEVEN: TAMADUNI ZA KIZUNGU ZINAJENGA UASHERATI NA MMOMONYOKO WA MAADILI, UAFRIKA UNAKUZA DINI NA MAADILI

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amewahimiza vijana wa nchi hiyo watafute nafasi za kujiendeleza kiuchumi na kupata nafasi za ajira, badala ya kujikita katika kuenzi tamaduni za Wazungu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha la utamaduni katika Chuo Kikuu cha Busitema mwishoni mwa wiki, Bw Museveni alisema ingawa tamaduni nyingi za Ulaya zinaonekana za kisasa, utamaduni wa Kiafrika unakuza dini na nidhamu.

“Nahimiza vijana wa Uganda na Afrika kwa jumla wajiepushe na tamaduni za kimagharibi ambazo zinawavuta zaidi katika usherati na mmomonyoko wa maadili,” akasema.

Rais Museveni aliwakumbusha wanafunzi chuoni humo na wageni waliohudhuria kwamba sheria ya kupiga marufuku ushoga na usagaji inatumika.

Kwa hivyo aliwahimiza wananchi kote Uganda, wawe wakiwaripoti watu watakaowapata au kuwashuku kuwa wanavunja sheria hiyo na kujihusisha na ushoga ama usagaji.

Sheria hiyo inayopiga marufuku ushoga na usagaji inatoa adhabu kali ikiwemo kifungo cha maisha gerezani kwa wanaopatikana na hatia.

Mwezi uliopita Rais Museveni alitia saini muswada wa sheria ya kupiga marufuku ushoga na usagaji ambapo mataifa mengi ya Ulaya na Marekani yaliipinga na hata kutishia kusitisha misaada kwa Uganda.


Lakini Rais Musebveni alisema maadili ya Waafrika ni muhimu kuliko misaada ambayo baadaye itafanya Afrika ipoteze mila na tamaduni zake.

Yoweri museven