Wednesday, 19 March 2014

MAIMAMU JORDAN WATANGAZA KUGOMA KUISHINIKIZA SERIKALI KUTOAJIRI MAIMAMU WA NJE YA NCHI

Mamia ya maimamu nchini Jordan wametishia kugoma na kuacha kutoa khutba za ijumaa kama serikali ya nchi hiyo itaendelea na mpango wake wa kuajiri maimamu kutoka nchi ya Misri.

Dhiab Abu Seeni ambaye ni kiongozi wa kundi la maimamu alisema Jordan ina maimamu wenye sifa za kufanya kazi nchini humo kuliko kuchukua maimamu kutoka nchi nyingine. 

Aliendelea kusema kuwa bado wenye sifa za kuwa maimamu wapo wengi na hawana misikiti ya kuongoza ibada.

Aidha alisema wamepanga hatua ya kugoma kwa siku mbili nchi nzima katika siku za tarehe 31 machi na Aprili 7 kuonesha kupinga misimamo ya serikali ya kuajiri maimamu kutoka nje ya nchi.

Alisema hiyo ni hatua ya kuishinikiza serikali kuachana na mpango huo. Mwezi uliopita Wizara ya mambo ya dini ilitangaza mipango ya kuajiri Maimamu 50 kutoka nchini Misri. 

Waziri wa mambo ya dini, Hayel Dawoud amekosoa mpango huo wa mgomo badala yake amewataka maimamu kukaa chini na kuzungumza na Serikali.