Msikiti wenye utata mjini Mombasa, Masjid Mussa, umepewa jina jipya la Masjid Shuhadaa (Msikiti wa Mashahidi), limeripoti gazeti la The Standard la Kenya siku ya Alhamisi.
kumekuwepo kwa mkanganyiko juu ya yule anayehusika na utoaji huo wa jina jipya, kwani maafisa wa kaunti hawakuwa na uhakika ikiwa ni kamati ya msikiti huo au vijana wenye msimamo mkali.
Jina hilo jipya liliandikwa kwa maandishi ya wazi kwenye msikiti huo mahala palipokuwa na jina kongwe.
Mimbari ambayo ulamaa aliyeuawa Sheikh Aboud Rogo na na warithi wake waliwahi kuhutubia pia imerejeshwa.
Msikiti huo ulikuwa ni eneo la makabiliano makali kati ya polisi na vijana wanaoshukiwa kuwa na msimamo mkali mapema mwezi Februari.
Ulamaa Sheikh Abubakar Shariff Ahmed wa Mombasa, anayefahamika pia kama Makaburi, alisema anaunga mkono jina hilo jipya kwani linatoa heshima kwa maulamaa 15 ambao sasa ni marehemu na ambao walihusishwa na msikiti huo.
"Marehemu Aboud Rogo alikuwa akihutubu kwenye msikiti huu. Maulamaa wengine waliohusishwa na msikiti huu ni pamoja na Samir Khan, Sheikh Shaaban na Sheikh Ibrahim, ambao wote waliuawa," alisema Makaburi.
Maafisa walitishia kuufunga msikiti huo kutokana na madai ya kuwa na mahusiano na makundi ya misimamo mikali ya Kiislamu, lakini wakakubaliana kuuacha uendelee kufanya kazi chini ya kamati mpya.
Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Shariff Nassir, alisema kupewa jina kwa msikiti huo kusitumike kama kisingizio cha kulivamia tena jengo hilo.
