Mapigano yalizuka kati ya Waislamu na Wakristo magharibi mwa mji huo, ambapo nyumba kadhaa za Waislamu zimechomwa moto, mashuhuda na makundi ya misaada ya kibinadamu wamesema.
Adiha, raia wawili Waislamu wameuawa kiholela katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda katika tukio hilo, askari wa kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika alimuua mwanamgambo mmoja wa Kikristo aliyetaka kuuchoma moto mwili wa Muislamu aliyeuawa.
Nchi hiyo ilitumbukia katika ghasia mwezi Machi mwaka jana baada ya wapiganaji wa kundi la Seleka, lenye Waislamu wengi, walipomuondoa madarakani rais Francois Bozize, na kumuingiza madarakani Michael Djotodia. Bozize aliikimbia nchi hiyo baada ya kuondolewa badarakani.
Hata hivyo, nchi hiyo ilizidi kutumbukia katika ghasia zaidi baada ya makundi ya Wakristo wenye silaha kuanza kufanya mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi mwezi Desemba mwaka jana.
Ghasia hizo ziliendelea hata baada ya Djotodia kujiuzulu na bunge kumteua Bi. Catherine Samba Panza kuwa rais wa mpito.
Maelfu ya Waislamu wameikimbia nchi hiyo kuepuka mauaji na uporaji unayofanywa na wanamgambo wa Kikristo ambao wanadai kulipiza kisasi.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi, watu wapatao 9,000 wamekimbilia mashariki mwa Cameroon ndani ya siku 10 pekee.
Zaidi ya Waislamu 4,000 wamekimbilia katika uwanja wa Ndege wa Bangui, karibu na kambi za jeshi la Ufaransa na vikosi vya Umoja wa Afrika, wakitarajia kuondoka nchini humo ndani ya wiki chache zijazo.
Mwezi Desemba Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kupelekwa kwa vikosi vya kimataifa kwa ajili ya ulinzi wa amani, ambapo Ufaransa na Umoja wa Afrika walipeleka vikosi hivyo.
