Wednesday, 12 February 2014

WANAMGAMBO WA KIKRISTO WA ANT-BALAKA WAPEWA ONYO KUACHA KUHATARISHA USALAMA WA RAIA NCHINI JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amevitolea wito kikosi cha Ufaransa na kile cha Umoja wa Afrika kukomesha vitendo vya kikatili vinavyotekelezwa na kundi la wakristo la Ant-balaka.

"Kama itahitajika kutumia nguvu ili kukomesha vitendo vya kikatili vinavyotekelezwa na kundi la Anti-balaka, majeshi ya Ufaransa na yale ya Umoja wa Afrika yanapaswa kutumia sheria ya Umoja wa Mataifa ya kumaliza kundi hilo", amesema waziri Le Drian.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean Yves Le Drian anafanya ziara katika nchi kadhaa barani Afrika.

Aliyazungumzia hayo juzi alipokua mjini Brazzaville, nchini Congo, juu ya mzozo wa jamhuri ya Afrika kati, amesema majeshi ya Ufaransa yataendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha Amani inarejea nchini humo.

“Msimamo wa ufaransa nchini Bangui unaeleweka”, alisema LeDran, akibainisha kwamba lengo la Ufaransa ni kufanya kila jitihada ili amani ya kudumu irejee nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

“Hasa kuyapokonya silaha makundi yanayozimiliki bila kuegemea upande hata mmoja, huku serikali ya mpito ikiendelea na shughuli zake ili amani irejee, na hali ya kibinadamu iweze kuwa sawa”, aliendelea kusema waziri huyo wa Ufaransa.

Le Drian alianza ziara hiyo ya kikazi tangu jumapili katika kanda ya Afrika ya Kati ili kuzungumzia jitihada za jeshi la Ufaransa kurejesha hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Le Drian anatazamiwa kuendelea na ziara yake hadi mjini Bangui hapo leo.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian