Jenerali Soriano ametangaza kuwa, wanamgambo wa Anti-Balaka wamekuwa wakiwashambulia Waislamu na kufanya vitendo vinavyokinzana na sheria na hivyo kuzidi kuvuruga hali ya usalama na amani katika nchi hiyo.
Matamshi ya jenerali huyo wa Kifaransa yanatolewa katika hali ambayo, Peter Bouckaert Mkuu wa Masuala ya Dharura katika Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch naye ameonesha wasiwasi mkubwa alionao kutokana na kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kusema kwamba, yamkini Waislamu wote wa nchi hiyo wakalazimika kuikimbia nchi yao.
Peter Bouckaert amesema katika ripoti yake kwamba, baadhi ya makazi ya Waislamu yamebakia tupu kutokana na watu wake kulazimika kuyakimbia makazi hayo wakihofia usalama wa maisha yao.
Ripoti ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch inaonesha kwamba, nyumba za Waislamu zinaendelea kubomolewa na inaonekana kwamba, kuna njama zilizoko nyuma ya pazia za kuwaangamiza kabisa Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Waislamu wanaunda asilimia 15 ya wakazi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Makumi ya maelfu ya Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekimbilia katika nchi za Cameroon na Chad na kuomba hifadhi katika nchi hizo.
Aidha kuna raia wengi ambao wamekusanyika kwenye kambi za karibu na uwanja wa ndege katika mji mkuu Bangui na idadi yao imekuwa ikiongezeka kila siku.
Hivi karibuni Waislamu wawili walinyongwa na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka, kitendo ambacho kilizidi kudhihirisha kilele cha vitendo vya kinyama vya wanamgambo hao dhidi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu.
Akizungumzia kiitendo hicho cha kikatili dhidi ya Waislamu hao, Andre Nzapayeke, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alisema, unyama huo ni pigo kubwa kwa serikali.
Rais Catherine Samba-Panza wa nchi hiyo alikitaja kitendo hicho cha kinyama kwamba, ni cha kutia simanzi. Kushtadi mgogoro katika mji mkuu Bangui na maeneo mengine ya nchi hiyo kunaripotiwa katika hali ambayo, Ufaransa imetuma majeshi yake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa madai ya kwenda kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo.
Kwa sasa kuna wanajeshi elfu moja na mia sita wa Ufaransa na takribani askari elfu tano wa Kiafrika wako huko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wakifanya hima ya kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kutokana na kuwa Waislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaunda sehemu muhimu ya uchumi wa nchi, kuondoka kwao kutakuwa na taathira hasi kwa uchumi wa nchi hiyo.
![]() |
| Jenerali Francisco Soriano |
