Wednesday, 5 February 2014

VIONGOZI WA MOMBASA WALAANI FUJO ZA MSIKITINI, WAPINGA MISIKITI KUFUNGWA

VIONGOZI wa Mombasa wameshutumu vikali ghasia zilizotokea katika msikiti wa Masjid Musa, Mombasa Jumapili na kutaka waliohusika kukamatwa na kushtakiwa.

Wakiongozwa na Seneta wa Mombasa Omar Hassan, viongozi hao walitaja ghasia hizo kama sizizofaa na wakawataka maafisa wa usalama kutia juhudi zaidi kuhakikisha kuwa usalama umeimarishwa katika eneo hilo.

Viongozi hao walisema kuwa hawatavumilia vikundi fulani vinavyojihusisha na visa vya uhalifu na kuongeza kuwa usalama wa kila Mkenya ni lazima ulindwe kwa mujibu wa katiba mpya.

“Sisi kama viongozi hatutagawanywa na vitendo vya vikundi fulani. Tulichaguliwa kuwahudumia wakazi wote wa Mombasa na sheria lazima zifuatwe,”alisema Bw Hassan.

Aidha viongozi hao walikosoa mbinu za serikali za kupambana na vikundi haramu na kuongeza kuwa mbinu hizo huenda zikachochea ghasia zaidi. “Njia zinazotumiwa na serikali katika juhudi za kukomesha vikundi harama hazifai na lazima ibadilishe mbinu hizo ili kuhakikisha usalama wa wananchi wasiokuwa na hatia umelindwa,” alisema.

Wakati huo huo, viongozi hao walielezea hofu yao kuhusu madai ya serikali kukusudia kufunga baadhi ya misikiti kama mojawapo wa njia za kupambana na uhalifu. “Tunatumai kuwa taarifa hizo si za kweli kwa sababu hakuna serikali ambao ina kibali za kuingilia masuala ya kidini,” alisema Bw Hassan.

Seneta wa Mombasa Omar Hassan