Thursday, 27 February 2014

SERIKALI YA SOMALIA YAELEZA MPANGO WA KUPAMBANA NA UGAIDI

Waziri Mkuu wa Somalia Abdiweli Sheikh Ahmed عبدالولي الشيخ أحمد siku ya Jumanne alieleza mpango wa usalama wa serikali yake kufuatia shambulizi la wiki iliyopita katika Villa Somalia.

"Hatua ya haraka itachukuliwa huko Mogadishu na zaidi ya hapo ili kusambaratisha mitandao ya magaidi na kuzuia mashambulizi mengine," Ahmed alisema katika taarifa.

Serikali iliteua timu ya uchunguzi inayojumuisha baraza la mawaziri na wataalamu ili kuangalia matukio yanayosababisha mashambulizi.

Pia ilianzisha kikosi kazi kinachojumuisha wawakilishi kutoka Baraza la Mawaziri, bunge, vikundi vya vyama vya kiraia, uongozi wa wilaya, jumuiya ya wafanyabiashara, polisi, intelijensia, viongozi wa dini, vikundi vya wanawake na vijana, ili kushughulikia usalama ngazi ya wilaya, na kuwezesha ushirikiano kati ya serikali na raia ili kuziweka salama jamii za wenyeji.

Serikali inapanga kuteua kamati ili kutathmini uwezo na utendaji wa mashirika ya usalama, na sasa inaandika sheria za kupambana na ugaidi zitakazowasilishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.

"Natoa wito kwa umma kushirikiana nasi na kuyasaidia mashirika ya ulinzi katika jitihada zao za kuhakikisha usalama kwa kuyatahadharisha mashirika husika kuhusu shughuli zozote wanazozitilia shaka", Ahmed alisema na kuongeza, "Pia viongozi wa dini wana jukumu muhimu la kuuelimisha umma kuhusu hatari ya ugaidi na kwamba ni kinyume na mafundisho ya Uislamu ya kuua watu wasio na hatia."

"Hebu niseme tena madhara ambayo Al-Shabaab inasababishia nchi yetu tukufu na watu wetu wasio na hatia, tunapaswa sote kuungana pamoja kwa kuwa kupitia hatua ya pamoja tutalitokomeza kundi hilo la ugaidi", alisema.


Abdiweli Sheikh Ahmed