Uchunguzi wa milipuko umethibitisha kwamba mshukiwa wa Al-Shabaab aliyeuawa na polisi siku ya tarehe 1 Februari alihusika na kumuua askari wa kupambana na ugaidi, Ahmed Abdalla Bakhshwein, mwezi Januari, polisi nchini Kenya ilisema mjini Malindi siku ya Alhamisi.
Mtu huyo anayetuhumiwa kuwa mwanachama wa Al-Shabaab, Ali Mohamed Delawa, alipigwa risasi na afisa mmoja wa polisi mjini Malindi na alipatikana na bunduki aina ya Colt 45mm na risasi sita, liliripoti gazeti la The Standard la Kenya.
Uchunguzi wa silaha na risasi hizo ulimuunganisha Delawa na mauaji ya Bakhshwein ya tarehe 28 Januari na mashambulizi mengine kadhaa ya bunduki na maguruneti mjini Kwale, walisema polisi.
"Wataalamu wa uchunguzi wamethibitisha kwa hakika kwamba bunduki iliyopatikana kutoka kwa majambazi waliyopigwa risasi ni ile iliyotumika katika mashambulizi ya Malindi, Kwale na Diani," alisema Ofisa wa Idara ya Upepelezi wa Jinai ya Wilaya ya Malindi, John Ndungu, akimuelezea Delawa kama mmoja wa waliokuwa kwenye orodha ya wahalifu wanaosakwa sana.
Bunduki hiyo inaaminika kuwa iliibiwa kutoka kwa wanajeshi wa Kikosi Maalum cha Marekani nchini Somalia katika miaka ya 1990.
