Kuachiliwa huru kwa wafungwa hao kutoka jela ya Bagram kunatarajiwa kuharibu zaidi uhusiano ambao tayari ni mbaya kati ya Kabul na Washington huku wanajeshi wanaoongozwa na Marekani wakijitayarisha kuondoka baada ya miaka 13 ya kupigana na Kundi la Taliban.
“Wafungwa 65 waliachiliwa huru na kuondoka jela la Bagram leo asubuhi,” afisa wa shirika la serikali la mageuzi Afghan, Abdul Shukor Dadras, alisema.
Kabla ya kuachiliwa, jeshi la Marekani lilisema wapiganaji hao 'ni watu hatari' waliohusika na mashambulizi yaliyosababisha vifo na majeruhi kwa wafanyakazi 32 wa NATO na raia 23 wa Afghan.
Lakini Rais Hamid Karzai ametaja jela kama 'kiwanda cha kuzalisha taliban' na kudai kuwa baadhi ya wafungwa waliteswa ili kuchukia nchi yao.
Luteni Jenerali Ghulam Farouq, mkuu wa polisi ambaye anaendesha jela ya Bagram, alithibitisha kuwa wapiganaji hao wameachiliwa huru.
“Walitoka nje ya jela na kuingia kwenye magari yao na kisha kuelekea nyumbani kwao,” alisema na kuongeza, “Tuliwaachilia huru na ni jukumu lao wenyewe jinsi walivyoondoka. Hatukuwatayarishia usafiri".
![]() |
| Rais Hamid Karzai |
