Thursday, 6 February 2014

POLISI YA KENYA YADAI KUGUNDUA USHAHIDI WA UHALIFU KATIKA UVAMIZI WA MSIKITI MOMBASA

Polisi nchini Kenya wamepata nyaraka kadhaa na ushahidi mwengine kutoka kwenye Msikiti Mussa wa Mombasa, wanaokisia kuwa itawachukua miezi miwili au zaidi kuupitia, liliripoti gazeti la The Standard la Kenya siku ya Jumanne (tarehe 4 Febuari).Vitu vilivyopatikana ni pamoja na bunduki moja aina ya AK-47, mapanga na vifaa vingine vya vyuma, bendera za jihadi, vitabu, ramani, tarijisi, picha, taarifa juu ya watu wanaotuhumiwa kuwa majasusi na "Wasaliti wa Waislamu", na kitini cha mafunzo ya kigaidi.

Waraka moja uliopatikana unasemekana kuwa orodha ya majina ya wanamgambo kote Afrika ya Mashariki, kukiwa na marejeo ya mpaka Burundi.

Polisi pia walipata mkanda wa redio unaowatolea wito wapiganaji wa kujitolea wa Kiislamu kufanya mashambulizi kwenye nchi zinazowakandamiza Waislamu wa Somalia, ikifahamika kumaanisha nchi zinazochangia wanajeshi kwenye Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, na walikamata zaidi ya mikanda 200 ya CD na kadi za kuhifadhia zenye picha za kambi za mafunzo ya jihadi nchini Somalia na Syria na maelekezo ya sauti kuhusu matumizi ya silaha ndogo ndogo, uvamizi na itikadi.

"Tutahitaji miezi miwili kupitia mikanda hii ya CD na nyaraka," alisema Kamanda wa Polisi wa Mombasa, Robert Kitur.

Pia miongoni mwa mambo yaliyokamatwa ni kompyuta tatu za mkononi, ambazo zimepelekwa kwenye Kitengo cha Kupambana na Uhalifu wa Mitandaoni katika Idara ya Upelelezi wa Jinai kwa uchambuzi.

Kamanda wa CID wa Mombasa, Henry Ondiek, alitetea uvamizi wa Masjid Mussa, ambao baadhi ya viongozi wa Kiislamu wameukosoa kama ni udhalilishaji wa mahala patakatifu.

"Ukiangalia sheria ya makosa ya jinai na nyaraka nyingine za kisheria nchini Kenya, hakuna popote (panaposema) polisi wanazuiwa kuingia kwenye eneo ambako uhalifu kama ugaidi unafanyika," alisema. "Tutaendelea kuivamia misikiti na popote ambako uhalifu wa hali ya juu kama vile kupanga mashambulizi dhidi ya watu wasio na hatia unapangwa."

Robert Kitur