Mwendesha Mashtaka mkuu wa serikali, Alexander Muteti, alimuomba Jaji Edward Muriithi ampe hadi Alhamisi aweze kurudi mahakamani na maelezo kamili kuhusu aliko Hemed Salim Hemed.
Muteti alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Keriako Tobiko, Insketa Mkuu wa Polisi David Kimaiyo na Huduma ya Kitaifa ya Polisi, ambao wameshtakiwa kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Masoud Salim Hemed, nduguye mdogo Bw Hemed.
“Tumekubaliana na wakili wa mlalamishi kwamba kesi itasikilizwa Alhamisi, Februari 20, ili niweze kutoa maagizo fulani kwa polisi kwa ajili ya kutayarisha majibu kamili,” alisema Muteti.
Aliongeza kusema kuwa, “Mpelelezi anayechunguza kesi ya msikiti Musa aliniletea stakabadhi kwa niaba ya washtakiwa wa pili na wa tatu na haikuwa na majibu ya maswala yote yaliyo kwenye stakabadhi ya mlalamishi".
Hata hivyo, wakili huyo wa serikali aliiambia mahakama pasipo kunukuliwa kwamba polisi tayari wamekana kumkamata Bw Hemed kabla ya jaji kumfahamisha kuwepo kwa agizo lake la siku ya Ijumaa lililotolewa baada ya mahakama kukubali kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Hemed alikamatwa na polisi kwa mujibu wa picha zilizoambatanishwa na stakabadhi za kesi.
“Kama alikamatwa na polisi kama inavyodhihirishwa kwenye stakabadhi ya kesi, basi kuna uwezekano alipotea,” alieleza Jaji Muriithi.
Muteti akajibu: “Kama huyu bwana yuko katika kituo chochote cha polisi hapa nchini, mheshimiwa Jaji nitafanya hima kuhakikisha ameletwa kortini au kutoa maelezo ya kina kuhusu aliko. Nitafurahi kuwafikisha maafisa wahusika mahakamani kujibu maswali yote.”
Wakili wa mlalamishi, Bw Yusuf Abubakar, aliambia Jaji Muriithi kwamba mteja wake na shirika la Haki Afrika wamemtafuta Hemed katika vituo vyote vya polisi katika jimbo la Mombasa bila kufanikiwa.
“Polisi hawawezi kusema hawajamkamata ilhali kuna ushahidi wa kuonyesha walimtia nguvuni,” alieleza Abubakar.
Wiki iliyopita mahakama iliwaachilia huru zaidi ya watu 33 waliokuwa wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo ambapo afisa mmoja wa polisi aliripotiwa kuuawa.
Awali, mahakama hiyo hiyo iliagiza watoto wenye umri wa chini ya miaka 12 waliokuwa wamekamatwa waachiliwe huru.
![]() |
| Hemed Salim Hemed anayedaiwa kupotea |
