Kwa mara ya kwanza Jenarali huyo alifichua kuwa miili ya magaidi hao, waliouawa Jumatatu Septemba 23, 2013, ilitwaliwa na kikosi cha majasusi wa Marekani cha FBI.
Maafisa wakuu wa kutoka vitengo mbali mbali vya usalama nchini Kenya Ijumaa walisema kuwa habari zilizopeperushwa kwenye redio, runinga na kwenye magazeti ya nchini Kenya yalipotosha na yaliwasilishwa bila kuzingatia maadili na sheria ya taaluma ya uanahabari.
Aidha, wakuu hao wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi Balozi Rachel Omamo, Mkuu wa Majeshi (KDF) Jenarali Julius Karangi, Inspekta Mkuu wa Polisi David Kimaiyo na Mkurugenzi wa Habari katika Wizara ya Habari na Mawasiliano Mary Ombara walisema wanahabari wa Kenya hawakuongozwa na 'uzalendo’ waliporipoti kuhusu mkasa huo.
Wakuu hao walizungumza kwenye kikao cha uzinduzi wa ripoti kuhusu namna matukio ya mkasa huo yaliripotiwa, kikao kilichoandaliwa katika hotel ya Hilton Nairobi. Ripoti hiyo ilitayarishwa na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK).
“Nilisikitika kuwa vyombo vyetu vya habari viliripoti kisa hicho kana kwamba walikuwa wakiwatukuza magaidi, hali ambayo ilifanya vikosi vyetu vya usalama kuonekana kana kwamba hao ndio walikuwa wa kulaumiwa kutokana na tukio hilo,” alifoka Bi Omamo.
“Kwa mfano ilikuwa kinyume cha maadili ya uanahabari kwa vyombo vya habari kuchapisha na kuonyesha picha za maiti na wahasiriwa katika mkasa huo bila kujali kuwa hatua hiyo insababisha madhara zaidi, kisaikolojia kwa familia za watu hao. Ilikuwa makosa kwa wanahabari kugeuza mkasa huo kuwa sinema ya Rambo,” aliongeza Waziri huyo alionekana mwenye hasira za mkizi.
Takriban watu 69 waliuawa kwenye mkasa huo huku wengine zaidi ya 3,000 wakipata majeraha mbali mbali. Kwa mara nyingine Jenerali Karangi aliwatetea wanajeshi wa KDF walioshiriki katika operesheni ya kupambana na magaidi waliohusika na shambulizi hilo shughuli za uokoaji akisema kuwa hawakupora mali kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari.
“Maafisa wangu hawakupora chochote kutoka Westgate kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kile maafisa wangu walichukua ni maji ya chupa ya kunywa”, alisema Karangi akiongeza kuwa pesa zote zilizopatikana na wanajeshi katika kituo hicho ziliwasilishwa kwa wenyewe.
Jenarali Karangi alimkaripia mtayarishi wa kipindi 'Jicho Pevu' Mohammed Ali kwa kuonyesha picha ya jinsi Wakenya walikuwa wakiuawa kinyama na magaidi hao.
“Kile ambacho mwanahabari huyo alikuwa akifanya ni kutukuza magaidi hao wanne,” alisema mkuu huyo wa KDF huku akikana madai kuwa magaidi hao walitoroka kupitia mtaro chini ya jengo la Westagate.
Kwa mara ya kwanza Jenarali huyo alifichua kuwa miili ya magaidi hao, waliouawa Jumatatu Septemba 23, 2013, ilitwaliwa na kikosi cha majasusi wa Marekani cha FBI.
Bw Karangi alisema kuwa vyombo vya habari mataifa ya magharibu huongozwa na maadili na uzalendo wanaporipoti mashambulizi ya kigaidi, akiotoa mfano wa shambulizi ya kigaidi katika jumba la Twin Tower, Marekani mnamo Septemba 9, 2001.
“Japo zaidi ya watu 3,000 walifariki katika mkasa huo, ulimwengi haukuonywesha maiti zao au hata watu waliojeruhiwa,” alisema Karangi.
Kwenye hotuba yake ilisomwa na Naibu Mkurugenzi wa CID Gedion Kimilu,Bw Kimaiyo pia alilaumu wanahabari kwa kile alichokitaja kama hatua yao ya kuvuruga eneo la uhalifu hali iliyotatiza uchunguzi kuhusu kisa hicho.
Lakini Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika la Habari la Nation, Linus Gitahi alitetea vyombo vya habari akisema vilijaribu kadri vilivyoweza ili kujuza Wakenya kuhusu yaliyojhiri kwenye makasa huo. Hata hivyo, aliungama kuwa baadhi ya wanahabari walipeperusha habari ambazo hawakuwa wamethibitisha kando na kuonyesha picha za kuogofya.
“Vyombo vya habari vilijaribu kuripoti matukio hayo lakini tunakubali kuwa tulikosea hapa na pale. Lakini, tulikuwa wepesi kuomba msamaha na kuwachukuliwa hatua wenzetu waliotenda makosa kama hayo,” akasema Bw Gitahi.
Alipendekeza kuwa siku zijazo mkasa kama huo ukitokea Serikali inapasa kubuni kituo cha habari ambapo kupitia kwacho vyombo vya habari vitakuwa vikipata habari sahihi ili kuzuia utoaji wa habari za uwongo.
![]() |
| Mkuu wa KDF Jenerali Julius Karangi |
