Friday, 14 February 2014

RADIO AMAN: KITUO CHA REDIO CHA KWANZA KINACHOONGOZWA NA WANAWAKE NCHINI SOMALIA

Kituo cha kwanza cha radio ambacho wafanyakazi wake ni wanawake kimefunguliwa nchini Somalia na kuanza kurusha matangazo yake.  

Radio Aman yenye makao yake mjini Mogadishu mji mkuu wa Somalia, ilifunguliwa rasmi hapo jana ambapo wafanyakzi wake ni wanawake. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, lengo la kuanzishwa radio hiyo ni kupaza sauti ya wanawake wa Somalia ili isikike katika kila pembe ya nchi hiyo.

Aidha imeelezwa kwamba, radio hiyo imeanzishwa ili kuwafikishia watu kilio cha wanawake wa Somalia ambao wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya ubakaji na utumiaji mabavu. 

Bi Farhiyo Farah Aoble ambaye ni mkurugenzi wa Radio  ya Wanawake ya Aman ya Somalia amesema kwamba, bila shaka watakabiliwa na changamoto kubwa hasa kutokana na kuwa, hiyo ni radio ya kwanza ya wanawake.

Amesisitiza kwamba, wameazimia kwa dhati kuzingatia masuala yanayowahusu wanawake, elimu, jamii, maendeleo na masuala ya afya ambayo yana taathira ya moja kwa moja kwa jamii. Inasemekana kwamba, wananchi wengi wa Somalia wanatumia radio kwa ajili ya kupata habari na kusikiliza vipindi mbalimbali vya burudani.