Thursday, 20 July 2017

NAKALA YA QURANI ILIYOANDIKWA NA MTUMWA MWAFRIKA MAREKANI YAONESHWA BEIRUT

Nakala ya Qur'ani Tukufu iliyoandikwa na mtumwa Mwafrika nchini Marekani inaoneshwa mjini Beirut Lebanon.
Rami al-Nimr, mfanya biashara Mpalestina anayeishi Beirut ameandaa maonyesho hayo ambayo pia yanajumuisha sanaa ya kaligrafia ya Kiarabu na nakala za zamani za Kiarabu.

Maonesho hayo yalianza Aprili na yataendelea hadi Oktoba, amesema al-Nimr.

Katika maonesho hayo kuna nakala ya Qur'ani iliyoandikwa na mtumwa Mwafrika nchini Marekani katika muongo wa 1740. 

Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, mtumwa huyo kijana alikuwa amenunuliwa na familia moja katika jimbo la Maryland. 

Alitoroka hapo na kisha na kukimbilia Pennsylvania ambako alikamatwa na kuswekwa jela alikoandika nakala hiyo ya Qur'ani, anasema Nimr. 

Mtumwa huyo pia alichora picha yake katika ukurasa wa kwanza wa Msahafu huo. 

Inadokezwa kuwa nakala hiyo iliandikwa kwa mkono na Ayub bin Suleiman Diallo ambaye alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu. Bin Suleiman alikuwa mtumwa kutoka Ufalme wa Futa Tora katika eneo la Afrika Magharibi ya leo. Kwa mujibu wa nyaraka za historia, Ayub bin Suleiman alikuwa Imamu wa msikiti kabla ya kutekwa nyara na Wazungu waliokuwa wakifanya biashara ya utumwa.