Tuesday, 27 June 2017

WAUAJI PWANI SI WAISLAMU-WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema watu wanaofanya mauaji mfululizo ya kinyama katika mkoa wa Pwani si Waislamu kama ambavyo baadhi ya wananchi wanahisi.

Karibu watu 40, ikiwamo makundi ya polisi wenye silaha, wameuawa kwenye wilaya tatu za Kibiti, Mkuranga na Rufiji katika mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa swala na Baraza la Idd el Fitr kitaifa kwenye Msikiti wa Riadha Moshi Mjini jana, Majaliwa alisema watu wanaoendesha mauaji hayo siyo Waislamu.

“Shekhe Mkuu na Mufti wa Tanzania, nizungumzie mauaji ya mkoa wa Pwani ambayo umeeleza katika risala yako,” alisema Majaliwa na kukumbusha "salamu za Bakwata pia zimeeleza kwa hisia kali kuhusu matukio ya kusikitisha ya watu wasio na hatia katika mkoa wa Pwani.”

“Tunachokifanya sasa ni kuhakikisha kwamba tunawapata wahalifu halisi ili kuepuka kuingiza watu wasiohusika, kama vile hao wenye hisia kwamba mauaji hayo yanafanywa labda na Waislamu.

Alisema kazi kubwa inayofanywa hivi sasa na vikosi vya usalama nchini ni kuchuja taarifa za nani hasa anashiriki kwenye matukio hayo ili kuhakikisha wahalifu halisi wanapatikana na kuepuka kuingiza watu wasiohusika.

Alisema anachoweza kuwaahidi Watanzania kwa wakati huu ni kwamba wahalifu hao hawatapata mahali pa kukimbilia na watakamatwa tu.

“Kazi kubwa inafanywa ya kuchuja nani hasa ana anashiriki kwenye jambo hili na tunashukuru sasa Watanzania wanatusaidia katika kutuambia nani na nani wanahusika," alisema Waziri Mkuu. 

“Kwa niaba ya waathirika wa mauaji hayo ya watu wasio na hatia, napokea salamu zenu za pole na kuahidi kuongeza kasi katika kuhakikisha kila anayehusika na mauaji hayo anafikishwa katika vyombo vya sheria.”

Alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa zitakazotusaidia kuwabainisha wahalifu halisi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.

Awali, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shekhe Salim Ahmed Abeid, alieleza masikitiko kuhusu matukio ya mauaji ya mkoani Pwani, na akiomba serikali kuongeza umakini zaidi katika kushughulikia tatizo hilo.

“Kuna watu wanaibuka na kutaka kuvuruga amani kwa kuishirikisha imani ya dini ya Kiislamu," alisema Shekhe Abeid, lakini "hakuna mafundisho ya dini ya Kiislamu yanaruhusu hayo zaidi ya kuamrisha mema na kukatazana mabaya.”

Akizungumzia mauaji hayo, Shekhe Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakari Zuber Bin Alli, alisema mauaji yanayoendelea mkoa wa Pwani siyo mafundisho ya dini ya Kiislamu na wala dini hiyo siyo ya kigaidi. 

“(Uislamu) ni dini ya amani na ugaidi unaweza ukafanywa na mtu yeyote,” alisema Mufti.

“Hakuna sehemu vitabu vinafundisha kumdhuru mtu au kuua mtu kwa kisingizio cha imani ya dini.”