Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ali amewataka waislamu wote nchini Tanzania kuiunga mkono Bakwata na kuacha kulaumu.
Amesema baadhi ya waislamu wamekuwa wakilaumu kwa muda mrefu bila ya kutoa ushauri wa nini kifanyike tabia ambayo haijengi bali inatengeneza nyufa zinazoharibu mshikamano wa waislamu.
Sheikh Zubeir amesema hii ni Bakwata mpya na lengo kuu ni kuwaunganisha waislamu wote pamoja na taasisi mbalimbali za kiislamu.
Aidha amesema waislamu waache kulaumu na badala yake watoe ushauri pale wanapoona hapako sawa.
"Milango ya bakwata ipo wazi kwa yeyote yule mwenye ushauri mzuri alete, rai nzuri alete, maoni ya maendeleo alete, isipokuwa hatutaki fitina, unafiki hatutaki," alisema Mufti.
Sheikh Abubakar Zubeir aliyasema hayo katika Baraza la Maulid lililofanyika jana kitaifa katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri mkuu Kassim Majaliwa.
Kuhusu maboresho ya uongozi wa Bakwata, Mufti alisema baraza limekuwa imara zaidi kwa kushirikisha taasisi zote za Kiislamu, jambo ambalo linaepusha misuguano isiyo na tija mara kwa mara.
Alisema baraza lina wasomi wa kada zote na kutaka Waislamu wenye mawazo na nia ya kujenga maendeleo ya Waislamu na taifa kwa ujumla, kujitokeza na ushauri wao utazingatiwa na kupewa nafasi stahili
Aidha Mufti aliwaeleza waislamu namna ambavyo Bakwata inavyoshirikiana na Taasisi mbalimbali kwa kusaidia Maandalizi na ufanikishaji wa mashindano ya kuhifadhi Qurani.
Alitolea mfano wa Taasisi ya Al-hikma iliyomualika Imamu wa
msikiti wa Makkah Sheikh Abdulrahman Al Sudais kwamba yeye ndiyo aliyoiandika barua ya mualiko licha ya kwamba mashindano hayo hayakuandaliwa Bakwata.
Hata hivyo Sheikh Sudais hakufika nchini bali ulifika ujumbe maalumu uliomuwakilisha.
Tangu kuchaguliwa kuwa Mufti wa Tanzania Juni 23, mwaka 2015, Sheikh Abubakar Zubeir amekuwa akisisitiza umoja kwa waislamu pamoja na kuiunga mkono Bakwata.