Friday, 3 November 2017

MUFTI MKUU: CHEO CHA SHEIKH MKUU NI KIMOJA TU TANZANIA

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Abubakar Ali Zubeir amesema kwa mujibu wa katiba na muongozo wa Baraza kuu la waislamu Tanzania (Bakwata) kwamba cheo cha Sheikh Mkuu ni kimoja na si vinginevyo.

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir
Amesema kumekuwa na makosa ya kuwaita Masheikh wa wilaya au mikoa kwamba ni Masheikh wakuu. 

Amesema cheo cha sheikh mkuu ni kwa mufti tu na masheikh wa wilaya au mikoa wafahamike kama sheikh wa wilaya au sheikh wa mkoa na wasiitwe sheikh mkuu wa wilaya au sheikh mkuu wa Mkoa.

Aidha amesema cheo cha mufti hakikuwepo huko nyuma bali kilianza wakati wa utawala wa Rais Ali Hassani Mwinyi pale alipomtangaza Sheikh Mkuu wa wakati huo marehemu Hemed bin Jumaa bin Hemed kwamba si tu ni Sheikh mkuu bali ni Mufti mkuu wa Tanzania.

Sheikh Abubakar Zubeir amesema hapo ndipo kilipoongezwa cheo hicho kwa Sheikh mkuu wa Tanzania.

Aidha amewataka waandishi wa habari baada ya ufafanuzi huo alioutoa waanze kuandika Sheikh wa Mkoa, Sheikh wa Wilaya na si Sheikh Mkuu wa Mkoa au Sheikh Mkuu wa Wilaya. 

Sheikh Abubakar Zubeir ameyasema hayo wakati anahojiwa katika kipindi cha kiislamu kinachorushwa katika televisheni ya Taifa ya TBC1.