Zaidi ya watu 7,000 katika mji wa Naqada uliopo kusini mwa nchi ya Misri walihudhuria mazishi ya mzee mmoja aliyeishi shimoni kwa takriban miaka 50.
Habari zinasema kuwa mzee huyo alifariki siku ya Ijumaa na kuvutia maelfu ya watu kuhudhuria mazishi yake kinyume na maisha yake ya upweke shimoni karibu na mfereji ndogo.
Kwa mujibu wa Mohammed Zouz, mmoja ya wakaazi wa maeneo hayo ni kuwa mzee huyo aliishi shimoni kwa miaka 52.
Aidha wakaazi wengi pia wamekiri kushangazwa na jinsi kulivyojitokeza waombolezaji wengi katika mazishi yake.
Wanawake walilia, huku wanaume kwa vijana wakibeba matawi ya mitende na kuelekea wote katika mahali pa kuzika.
Vyanzo vya habari vilithibitisha jina la mzee huyo ni Jad al-Karim Abdelrahim aliyeishi jijini Cairo katika miaka yake ya ujana .
Inaelezwa baada ya kukumbwa na maradhi ya kisaikolojia na kihoro alirudi katika mji wake na kuanza kuishi shimoni akiwa bila ya nguo na kujifunika kwa Blanketi tu.
Hata nyakati za mvua kunyesha na shimo hilo dogo kujaa maji hakutoka mpaka maji yalipokauka yenyewe.
Wakazi wengi wa mji huo walizoea kumsalimia na yeye akijibu salamu zao na wengine kumtaka awaombee kwa Mwenyezi Mungu jambo ambalo alilifanya.
Kilichokuwa kikiwashangaza wakaazi wa mji huo ni kwamba kila walipomsalimia alijibu salamu zao na kumtambua kwa jina kila aliyemsalimu kana kwamba aliwahi kumfahamu kabla.
Mara nyingi alionekana akila samaki aliovua mwenyewe na kuwapa majirani na kumwandalia kwa ajili ya chakula chake.
Pia inasemekana alikuwa haruhusu mtu kumpiga picha wala kukubali zawadi kutoka kwa watu na hakupenda kuzungumza na watu wala kujichanganya nao.
Baadhi ya wazee wa mji waliwashauri Madaktari kumfanyia tiba lakini walipompima waliona ni mwenye afya nzuri na akili iliyo sawa jambo ambalo liliwashangaza.
